Nyansaho Foundation Yazidi Kunyoosha Mkono Kwa Wahitaji

GEORGE MARATO TV
0



Na Mwandishi Wetu, Serengeti

Shirika la NYANSAHO FOUNDATION limeandika historia mpya katika sekta ya elimu Wilayani Serengeti baada ya kukabidhi zawadi mbalimbali kwa wanafunzi na walimu wa Shule ya Msingi Maganana, Kata ya Nyambureti, kufuatia kufanya vizuri kwa kiwango cha juu katika Mtihani wa Taifa wa Darasa la Nne mwaka 2025 kimkoa.

Katika matokeo hayo, shule hiyo ilipata daraja la “A”, hatua iliyoiweka miongoni mwa shule kinara katika mkoa na kuleta fahari kubwa kwa jamii ya Nyambureti na Wilaya ya Serengeti kwa ujumla.

Hafla ya utoaji zawadi ilifanyika katika viwanja vya shule hiyo huku ikiambatana na shamrashamra za wanafunzi waliokuwa wakishangilia mafanikio yao. 

Baadhi ya Wazazi, viongozi wa kijiji, kamati ya shule na wadau wa elimu walihudhuria kushuhudia tukio hilo lililojaa furaha na matumaini mapya.

Akizungumza mbele ya hadhira, mwakilishi wa NYANSAHO FOUNDATION alisema taasisi hiyo inaamini kuwa elimu ndiyo msingi wa maendeleo endelevu, na kwamba kuwazawadia wanafunzi na walimu ni njia ya kuonesha kuthamini juhudi na kuhamasisha wengine kuiga mfano huo.

“Tunataka watoto wa Serengeti wajue kuwa juhudi zao zinaonekana na zinatambulika. Daraja la A si jambo dogo. Ni matokeo ya nidhamu, bidii na mshikamano kati ya walimu, wanafunzi na wazazi,” alisema na kuongeza kuwa

"Mafanikio hayo yanapaswa kuwa chachu ya mabadiliko kwa shule nyingine katika kata hiyo na kuahidi kuendelea kushirikiana na wadau wa elimu kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia"


Walimu walipewa pongezi maalum kwa usimamizi mzuri wa taaluma, huku wakisisitiza kuwa mafanikio hayo yametokana na ushirikiano mzuri kati ya shule na jamii.

Mkuu wa Mkuu wa Shule ya Msingi Maganana alisema mafanikio hayo yametokana na mikakati madhubuti ya ufundishaji, ikiwemo vipindi vya ziada, tathmini za mara kwa mara na ushirikiano wa karibu na wazazi.

“Tumekuwa tukifanya tathmini za kila mwezi ili kubaini mapungufu mapema. Ushirikiano wa wazazi umetusaidia sana kuhakikisha wanafunzi wanakuwa na mazingira bora ya kujisomea,” alisema.
Wito kwa Jamii. 


Baadhi ya wazazi walitoa wito kwa taasisi nyingine na wadau wa maendeleo kuiga mfano wa NYANSAHO FOUNDATION kwa kusaidia shule za vijijini ambazo mara nyingi hukabiliwa na changamoto za miundombinu na vifaa vya kujifunzia.

Dira ya Mbele

NYANSAHO FOUNDATION imeahidi kuendelea kutoa motisha kwa shule zinazofanya vizuri pamoja na kusaidia kuboresha miundombinu ya elimu, ikiwemo madawati, vitabu na programu za kuwajengea uwezo walimu.

Mafanikio ya Shule ya Msingi Maganana yanatajwa kuwa ishara ya matumaini kwa watoto wa Serengeti, yakionesha kuwa hata shule za vijijini zinaweza kung’ara kitaaluma endapo kutakuwa na ushirikiano, nidhamu na uwekezaji katika elimu.

Kwa sasa, Jamii ya Nyambureti ina kila sababu ya kujivunia, huku macho yakielekezwa katika mitihani ijayo kwa matarajio ya kuendeleza rekodi hiyo ya ufaulu wa kiwango cha juu.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
Post a Comment (0)

#buttons=(Accept !) #days=(20)

Our website uses cookies to enhance your experience. Learn More
Accept !
To Top