Februari 2, 2026, Baraza la Madiwani la Manispaa ya Musoma limefanya kikao cha rasimu ya bajeti ya mwaka wa fedha 2026–2027 kwa lengo la kujadili ajenda mbalimbali zinazohusu mapato na matumizi ya Manispaa.
Kikao hicho kilifunguliwa rasmi na Meya wa Manispaa ya Musoma, Mheshimiwa Alex Nyabiti, ambapo wajumbe wa Baraza walipata fursa ya kuchangia hoja mbalimbali zenye lengo la kuboresha ukusanyaji wa mapato ya Manispaa.
Katika michango yao, wajumbe walihoji hali ya ukusanyaji wa mapato kutoka vibanda vilivyopo maeneo mbalimbali ya Manispaa, wakibainisha kuwa makusanyo hayo bado ni madogo ukilinganisha na idadi halisi ya vibanda vilivyopo.
Aidha, ilielezwa kuwepo kwa tofauti za ulipaji kodi, ambapo baadhi ya vibanda hulipa kodi ndogo huku vingine vikitozwa kodi kubwa.
Vilevile, suala la leseni za biashara kwa vibanda lilipewa uzito, ambapo ilisisitizwa kufuatiliwa kwa karibu ili kuongeza mapato ya Manispaa. Kufuatia hilo, Mkurugenzi wa Manispaa ya Musoma alieleza kuwa ameunda Tume ya Uchunguzi itakayofuatilia leseni za biashara pamoja na vibanda vilivyopo katika maeneo yote ya Manispaa.
Aidha, wajumbe walibainisha kuwa ushuru wa samaki na dagaa bado uko chini ukilinganisha na kiwango cha uzalishaji kilichopo, sambamba na kodi ya majengo ambayo nayo imeelezwa kuwa ni ndogo ikilinganishwa na idadi ya majengo yaliyopo ndani ya Manispaa ya Musoma.
Katika hatua nyingine, Idara ya Maendeleo ya Jamii imeshauriwa kushirikisha wenyeviti wa mitaa katika utoaji wa mikopo kwa wananchi, ili kuhakikisha ushiriki mpana wa jamii na ufanisi wa mikopo hiyo.









