Na Angela Sebastian ;Bukoba
Mkuu wa mkoa wa Kagera kanali Yahya Ramadhan Kido amewaagiza wakala wa barabara Tanzania (Tanroads) na wakala wa barabara za mjini na vijijini (TARURA) mkoani humo,kuzingatia na kutoa kipaumbele katika masuala ya ajira kwa vijana na wanawake wakati wa utekelezaji wa miradi mbalimbali inayoendelea na inayotarajiwa kutekelezwa.
Ametoa agizo hilo leo wakati akifungua kikao cha bodi ya barabara cha kwanza tangu alipoteuliwa kuwa mkuu wa mkoa huo, kilichofanyika leo mjini Bukoba.
"Sasa nawaelekeza Tanroads na Tarura kuwahusisha kwa wingi jinsia ya kike katika fursa zilizopo ikiwa ni pamoja na vipaumbele kuajiri kundi la vijana kwani hii ndiyo nguvu kazi ya Taifa, tunayoitegemea hivyo sitegemei kuona mnaleta watu kutoka nje ya mkoa ambapo suala hili lilileta malalamiko kwa wananchi tunaowahudumia"ameagiza Kido.
Pia amewataka Tanroads na Tarura kuzingatia usimamizi mathubuti wa rasilimali fedha kwa maana asilimia ya kazi lazima ionekane thamani yake,ubora wa kazi kwa barabara zinazojengwa au kutengenezwa zidumu kuendana na matarajio na ushirikishwaji wa wananchi katika kulinda miundombinu ya barabara.
Wakati huo huo wajumbe wa bodi ya barabara hususani wabunge wameahidi kushikamana kwa nguvu moja na kuweka mkakati wa pamoja kuhakikisha fedha za ujenzi wa barabara zinatolewa kwa wakati ili kuwezesha miradi inayoendelea kukamilika kwa wakati na yenye viwango vinavyotakiwa.
Pia amemshukuru Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kumuamini na kumteua katika nafasi hiyo ambapo ameahidi kufanya kazi kwa uaminifu,weledi na kujituma ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma stahiki.
Wakati huo huo wajumbe wa bodi ya barabara hususani wabunge wameahidi kushikamana kwa nguvu moja na kuweka mkakati wa pamoja kuhakikisha fedha za ujenzi wa barabara zinatolewa kwa wakati ili kuwezesha miradi inayoendelea kukamilika kwa wakati na yenye Viwango vinavyotakiwa.
Joel Mwambungu ni meneja wa Tanroads mkoa wa Kagera ametaja changamoto wanazokumbana nazo kubwa ikiwa ni ufinyu na ucheleweshwaji wa fedha za matengenezo ya barabara,baadhi ya watu kuiba vifaa vya miundombinu ya barabara,wafanyabiasha wadogo kuvamia hifadhi ya barabara,mvua kukwamisha ujenzi kukamilika kwa wakati na vizuizi vya barabarani ambavyo havizingatii taratibu za barabara.
"Ili kufanya matengenezo yanayokidhi viwango ya miundombinu ya barabara mkoa tunahitaji kiasi cha shl. bil 25.8 lakini kwa kawaida bajeti inayotengwa ukomo wake ni shl.bil 14.5 ambapo nazo haziletwi kwa wakati hari inayosababisha miradi mingi kutokamilika kwa wakati hivyo nawashauri wadau hasa wabunge wetu kuangalia namna ya kulisukuma hili"alieleza Mwambungu.
Mhandisi Johnston Mutasingwa ni mbunge wa jimbo la Bukoba mjini amesema ukiangali katika wasilisho la Tanroads inaonyesha kwa mwaka 2024/2025 Tanroads walipokea asilimia tano ya fedha yote na 2025/2026 asilimia saba maana yake kuna pesa katika bajeti zao nazo zilitolewa ili kulipa madeni ya nyuma naomba kupitia kikao hiki tuangalie namna ya kuwezesha bajeti kupanda kama mikoa mingine.
Naye Devotha Daniel, ni mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Kagera,amesisitiza umuhimu wa kuharakisha utekelezaji wa miradi ya barabara iliyopo Wilayani Kyerwa ili kurahisisha usafiri na usafirishaji wa bidhaa, hususani mazao ya wakulima, na kuchochea maendeleo ya Mkoa wa Kagera kwasababu inaunganisha Tanzania na nchi za Uganda na Rwanda.





