_Asema ni mradi unaoipa hadhi nchi, unaojali utu_
WAZIRI MKUU Dkt Mwigulu Nchemba amekagua Mradi wa Maji wa Miji 28 unaoendelea kujengwa wilayani Korogwe mkoani Tanga kwa thamani ya sh. bilioni 171.
Akizungumza na viongozi na wananchi waliofika kwenye eneo la tukio katika kijiji cha Mswaha Darajani, kata ya Mswaha leo jioni (Jumamosi, Februari 14, 2026), Waziri Mkuu amesema ameridhishwa na utekelezaji wa mradi huo na akasisitiza kuwa wananchi wanaoishi Mswaha ambalo ni jirani kabisa na eneo la mradi, wapewe kipaumbele cha kupata maji pindi utakapokamilka.
Waziri Mkuu ambaye yuko mkoani Tanga kwa ziara ya kikazi ya siku tano, amesema kuwa uwekezaji mkubwa umefanyika maeneo yote nchini kwa dhamiria ya kumaliza changamoto ya huduma ya maji kwa Watanzania wote.
“Leo tunakuja kuuona mradi ambao hata kwa kuungalia tu unafurahisha, ni mradi wenye hadhi ya kiongozi anayejali mambo ya maendeleo. Mheshimiwa Rais Dkt. Samia ameweka fedha hapa ili zisaidie wananchi wa Muheza, Handeni, Korogwe na Pangani,” amesema.
“Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ni Rais anayejali maendeleo ya wananchi wake, na haya siyo maneno tu! Ninyi mnaona shughuli zinavyoendelea. Huu ni mradi wenye hadhi ya nchi inayoendelea, mradi wa aina hii siyo wa kutatua matatizo tu, bali unaipa hadhi nchi, ni mradi unaojali utu wa kila mwana Tanga, Muheza, Korogwe na Pangani,” amesisitiza Waziri Mkuu.
Mapema, Waziri wa Maji, Jumaa Aweso alisema kuwa Wizara ya Maji inaendelea kutekeleza mkakati wa Gridi ya Taifa ya Maji ambapo kwa sasa Tanzania ina jumla ya mita za ujazo bilioni 126 za maji ambayo yatatumika ipasavyo kwa manufaa ya wananchi.
“Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alitupa maelekezo kwamba Wizara ya Maji tutumie utajiri wa vyanzo vya maji vilivyopo Tanzania kumaliza changamoto ya maji kwa Watanzania. Alisema hataki kuona mwanamke wa Kitanzania akihangaika kutafuta maji ndipo akaanzisha kampeni ya kumtua mama ndoo kichwani.”
Awali, akitoa taarifa ya mradi huo mbele ya Waziri Mkuu, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Mwajuma Waziri alisema kuwa Mradi wa Maji wa Miji 28 unachukua maji kutoka Mto Pangani na umesanifiwa kuhudumia wilaya za Handeni, Korogwe, Muheza na Pangani pamoja na vijiji 161 vinavyozunguka maeneo hayo.
“Mradi huu kwa sasa umefikia asilimia 76, utapokamilika kwa siku unatarajiwa kuzalisha lita milioni 51 za maji yaliyosafishwa na kuwanufaisha moja kwa moja wakazi zaidi ya 868,000 katika maeneo yaliyolengwa,” alisema.
Mradi huo unaosimamiwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira wa Handeni Trunck Main (HTM) unalenga kuongeza uwezo wa uzalishaji wa maji kutoka wastani wa lita milioni 5.5 kwa siku hadi kufikia lita milioni 52 kwa siku. Lengo ni kukidhi mahitaji ya maji kwa kipindi cha miaka 20 ijayo kwa wakazi wa miji ya Korogwe, Handeni, Muheza na Pangani.
Jumla ya watu 870,629 wanatarajia kunufaika na mradi huo wakiwemo wakazi 130,843 wa Korogwe, Handeni (546,680), Muheza (142,711) na Pangani (50,395).





