*Kutoka: Dawati la Habari Polisi Mwanza*
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza limewafikisha mahakamani dereva wa gari la abiria T. 234 BUM aina ya Toyota Hiace pamoja na mmiliki wake, kufuatia ajali ya barabarani iliyosababisha kifo cha askari wa Kikosi cha Usalama Barabarani Wilaya ya Nyamagana, Coplo Tumsifu Kileo, aliyekuwa akitekeleza majukumu yake, pamoja na kumjeruhi mtembea kwa miguu, Lucia Rweikiza.
Washtakiwa hao ni Mohamed Rashid Mumba (40), mmiliki wa gari hilo na Alphonce Fredrick Kashozi (25), dereva wa gali hilo (daladala), ambao wamefikishwa leo Februari 20, 2026 katika Mahakama ya Wilaya ya Nyamagana na kusomewa mashtaka nane yanayowakabili.
Akisoma shauri la jinai namba 3749 la mwaka 2026 mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Mahakama ya Wilaya ya Nyamagana, Clement Tuji, Wakili wa Serikali, Stella Minja, alianza kwa kumsomea mshtakiwa wa kwanza, Mohamed Rashid Mumba, ambaye anakabiliwa na mashtaka matatu.
Shtaka la kwanza ni kushindwa kutunza kumbukumbu za dereva wake, kinyume na kifungu cha 93 na 127(1) cha Sheria ya Usalama Barabarani, Sura ya 168, mapitio ya mwaka 2023.
Shtaka la pili ni kumruhusu dereva kuendesha gari katika barabara ya umma likiwa na hitilafu, kinyume na kifungu cha 39(6)(a), (b) na (c) cha sheria hiyo, ambapo kioo cha dashibodi kilikuwa kimevunjika, mlango wa mbele wa abiria ulikuwa umeharibika na gari halikuwa na mikanda miwili ya usalama kwa dereva na abiria.
Katika shtaka la tatu, mshtakiwa huyo anakabiliwa na kosa la kumruhusu dereva kuendesha gari bila kuwa na leseni, kinyume na kifungu cha 24(2) na 127(1) cha Sheria ya Usalama Barabarani.
Kwa upande wa mshtakiwa wa pili, Alphonce Fredrick Kashozi (dereva), anakabiliwa na mashtaka matano.Shtaka la nne ni kusababisha kifo kwa kuendesha gari kwa hatari kwa mwendo kasi katika barabara ya umma, kinyume na kifungu cha 49 na 75(2)(a) cha Sheria ya Usalama Barabarani, Sura ya 168, marejeo ya mwaka 2023.
Shtaka la tano ni kusababisha majeraha kwa kuendesha gari kwa hatari na kumgonga Lucia Rweikiza (31), mkazi wa Mahina, jijini Mwanza, kinyume na vifungu vya 49 na 75(2)(a) vya sheria hiyo.
Kosa la sita ni kuendesha gari bila kuwa na leseni, kinyume na kifungu cha 24(1) na 127(1) cha Sheria ya Usalama Barabarani, wakati kosa la saba ni kuendesha gari lenye namba za usajili T.203 BUM aina ya Toyota Hiace likiwa na hitilafu, kinyume na kifungu cha 45(1) na 5 cha sheria hiyo.
Kosa la nane ni kushindwa kutoa taarifa ya ajali katika kituo chochote cha polisi mara baada ya kusababisha ajali hiyo, kinyume na kifungu cha 68(2)(b) na 75(2)(d) cha Sheria ya Usalama Barabarani.
Mahakama iliwataka washtakiwa kuwa na wadhamini wawili kila mmoja, kusaini bondi ya shilingi milioni tatu kila mmoja, pamoja na kuwasilisha barua za dhamana kutoka serikali za mitaa. Hata hivyo, walishindwa kutimiza masharti hayo.
Wakili wa Serikali, Stella Minja, aliomba mahakama kutoruhusu dhamana kwa washtakiwa hao akieleza kuwa mdhamini wa mshtakiwa wa pili ni mkazi wa Wilaya ya Ilemela lakini nyaraka zake hazikuthibitishwa na Mahakama ya Wilaya ya Ilemela, huku kila mshtakiwa akiwa na mdhamini mmoja tu.
Kutokana na mapungufu hayo, maombi ya dhamana yalishindikana.
Minja pia aliomba mahakama ipange tarehe nyingine kwa ajili ya kusomewa hoja za awali, akieleza kuwa upelelezi wa shauri hilo umekamilika.
Hakimu Mkazi Mwandamizi, Clement Tuji, ameahirisha shauri hilo hadi Februari 25, 2026, huku washtakiwa wakiendelea kushikiliwa rumande.



