Na mwandishi wetu Jovina Massano.
Chemba ya Taifa ya Biashara (TNCC) ambayo hapo awali ilifahamika kama TCCIA kuunganisha mifumo yake na Serikali ili iweze kusomana na kubadilishana taarifa kwa ufanisi hapa nchini.
Hatua hiyo inalenga kupunguza urasimu katika utoaji wa huduma na kuimarisha mazingira ya Biashara kupitia maboresho ya teknolojia hiyo.
Katika kuhakikisha mageuzi hayo yanafanikiwa kwa kiasi kikubwa, Chemba ya Taifa ya Biashara(TNCC) imezindua mafunzo ya wiki moja mkoani Mbeya yanayohusu matumizi ya mfumo mpya wa utoaji wa Vyeti vya Uasili (Certificate of Origin) kupitia Tanzania Chamber Portal (TCP).
Mafunzo hayo yanahusisha mikoa 14 ikiwemo Ruvuma, Morogoro na Dodoma, yakilenga kuwajengea uwezo viongozi wa TNCC pamoja na wafanyabiashara ili waweze kutumia mfumo huo kwa ufanisi.
Mfumo huo utaongeza uwazi, kupunguza urasimu na kuharakisha utoaji wa huduma kwa wafanyabiashara, huku ukiunganisha moja kwa moja mifumo ya TNCC na Serikali kwa ufanisi zaidi.
Akiongea katika mafunzo hayo Mwenyekiti wa TNCC Mkoa wa Mbeya Bw. Erick Sichinga amesema wafanyabiashara wa mkoa huo wanakwenda kunufaika kwa kiasi kikubwa kwa kupunguza ghalama na kuokoa muda kupitia mfumo huo mpya.
“Kwa wafanyabiashara wa Mkoa wa Mbeya, mfumo huu utapunguza gharama na muda wa kufuatilia Vyeti vya Uasili hasa kwa wanaojihusisha na biashara za mipakani na masoko ya nje kupitia mfumo huu wa kidigitali tutakuwa na uhakika wa ushindani bora zaidi kikanda na kimataifa huku tukiongeza ufanisi na uwazi katika shughuli za biashara.”amesema Erick.
Mafunzo hayo yanaratibiwa na TNCC kwa udhamini wa TradeMark Africa kwa kushirikiana na Serikali kupitia TRA, ikiwa ni sehemu ya mkakati mpana wa kuifanya Tanzania kuwa na mifumo ya kisasa jumuishi na rafiki kwa biashara za kikanda na kimataifa.
Nae Afisa forodha Tunduma wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bw. Gwakisa Mwaikenda amesema mfumo huo shirikishi utaimarisha ukusanyaji wa mapato na kuziba mianya ya upotevu wa mapato kupitia ufuatiliaji wa kidigitali.
Ni vema wafanyabiashara hapa nchini kuhakikisha wanashiriki kikamilifu katika fursa za mafunzo zinazotolewa na Chemba ya Biashara ya Taifa( TNCC) kwa kuwa ndio taasisi inayowasimamia na kujiunga ili kunufaika kibiashara na kupunguza sintofahamu katika utekelezaji washughuli zao kibiashara.





