📍SEKTA YA FEDHA YAKUA, YAONDOLEWA KWENYE ORODHA YA MATAIFA HATARISHI
Na Mashaka Mhando, Tanga
SEEIKALI ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetangaza mafanikio makubwa katika sekta ya fedha, huku rasilimali za kibenki zikipaa hadi kufikia shilingi trilioni 71.8 na nchi kuondolewa rasmi katika orodha ya mataifa yenye vihatarishi vya kifedha (Grey List) duniani.
Hayo yamebainishwa na Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Laurent Deogratius kwa niaba ya Waziri wa Fedha Balozi Khamis Mussa Omar, wakati akifungua Maadhimisho ya Tano ya Wiki ya Huduma za Fedha Kitaifa yaliyofanyika katika Viwanja vya Usagara, jijini Tanga, Januari 21, 2026.
Akizungumza mbele ya mamia ya wananchi na wadau wa fedha, Naibu Waziri amesema kuondolewa kwa Tanzania kwenye orodha ya nchi hatarishi (High-Risk List) na Umoja wa Ulaya (EU) ni ushindi mkubwa utakaofungua milango ya uwekezaji na kurahisisha miamala ya kimataifa kuanzia Januari 29, 2026.
Takwimu zinaonesha kuwa sekta ya kibenki imeendelea kuimarika kwa kasi, ambapo amana za wateja zimeongezeka kutoka shilingi trilioni 42.7 mwaka 2024 hadi kufikia shilingi trilioni 50.2 mwezi Septemba 2025.
Aidha, mikopo kwa sekta binafsi imeshuhudia ukuaji wa asilimia 24, ikifikia shilingi trilioni 42 ikilinganishwa na shilingi trilioni 35 za mwaka uliopita, huku kiwango cha mikopo chechefu kikidhibitiwa vyema na kubaki asilimia 2.78, kiwango ambacho ni chini ya ukomo wa kisheria wa asilimia 5.
Katika kusaidia wajasiriamali wadogo, Naibu Waziri ameeleza kuwa Serikali imefanikiwa kutoa jumla ya shilingi bilioni 41.49 kwa wanufaika 10,288 ndani ya siku 100 pekee (Novemba na Desemba 2025) kupitia mifuko 76 ya uwezeshaji nchini.
Upande wa sekta ya bima nao umeonesha kishindo kikubwa, ambapo Naibu Kamishna wa Bima, Khadija Said, amebainisha kuwa uandikishaji wa ada za bima umekua kwa asilimia 20 na kufikia thamani ya shilingi trilioni 1.52
Khadija amesisitiza kuwa soko la bima limeendelea kutanuka likiwa na jumla ya wanufaika milioni 25.9, huku madai ya bima yaliyolipwa kwa wananchi waliofikwa na majanga yakifikia shilingi bilioni 545.4.
Kuhusu utekelezaji wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote, Mamlaka ya Usimamizi wa Bima (TIRA) imetangaza kusajili skimu saba za bima ya afya na vituo 8,500 vya kutolea huduma nchi nzima ili kuhakikisha kila Mtanzania anapata matibabu bila kikwazo cha fedha.
Sekta ya masoko ya mitaji na dhamana (CMSA) pia imeweka rekodi mpya, ambapo thamani ya uwezekaji imefikia shilingi trilioni 63.07, huku kukiwa na bidhaa mpya za kijani (Green Bonds) na hatifungani za kijamii zinazovutia wawekezaji wengi.
Kwa upande wa Hifadhi ya Jamii, ripoti inaonesha mifuko mitatu mikuu ina jumla ya wanachama milioni 3.05 ikiwa na thamani ya mali ya shilingi trilioni 25.56, jambo linalohakikishia usalama wa maisha ya baadaye kwa wafanyakazi.
Maendeleo ya kidijitali yamechangia kwa kiasi kikubwa huduma jumuishi za fedha kufikia asilimia 76 mwaka 2023, ikiwa ni ongezeko kutoka asilimia 65 ya mwaka 2017, shukrani kwa kukua kwa matumizi ya simu za mkononi na mawakala wa benki waliofikia 145,430.
Hata hivyo, Naibu Waziri huyo ametoa onyo kali dhidi ya wakopeshaji wasio rasmi maarufu kama "Mikopo Kausha Damu", na kuiagiza Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kuongeza udhibiti ili kuwalinda wananchi wasipoteze mali zao.
Waziri amewahimiza wananchi wa Tanga na Tanzania kwa ujumla kutumia wiki hii ya maadhimisho kujifunza kusoma mikataba ya fedha na kujiunga na taasisi zilizosajiliwa kisheria ili kuepuka hasara zisizo za lazima.
Maadhimisho haya ya Tano yanayofanyika Tanga ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango Mkuu wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha (2021/22-2029/30) unaolenga kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha biashara na fedha barani Afrika.
Awali Kaimu Mkuu wa mkoa wa Tanga na Mkuu wa wilaya ya Tanga, Dadi Kolimba alisema kwa upande wake akitoa salamu za mkoa huo alisema kuwa pato la mkoa kiuchumi limekuwa hadi kufikia sh Tril 9.3 mwaka 2024 kutoka sh Tril 6.8 mwaka 2020.
Huku pato la mtu mmoja mmoja likikuwa kutoka wastani wa sh Mil 2.7 mwala 2020 hadi kufikia Mil 3.4 mwaka 2024.










Comments
Post a Comment