Ada Ouko na Timothy Itembe, Musoma.
MFUKO wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSF) umeanza kulipa stahiki za watumishi mbalimbali wa umma wakiwemo ambao walioondolewa katika mfumo wa ajira kutokana na kuwa na vyeti feki.
Kaimu Meneja Pssf Mkoa wa Mara Nuru Mahinya amebainisha hayo wakati akifungua semina ya siku moja janury 22,2026 inayolenga kuwajengea waandishi wa habari mkoani humo namna kuripoti taarifa zinazohusiana na mfuko huo wa jamii.
"Tumieni kalamu zenu katika kufikisha ujumbe huu kwa jamii na katika hili tuna maana ya watumishi wale walioondolewa kazini kwa sababu ya vyeti feki tayari wamelipwa stahiki zao ambazo ni asilimia tano waliochangia kwenye mfuko huo wakati wa utumishi wao.alisema Nuru.
Alisema mfuko huo pia umeanza kulipa pensheni ya mkupuo wa miezi 36 mstaafu aliyefariki kundi hilo linalohusisha watumishi wa umma waliostaafu kwa umri au ugonjwa tu.
"Malipo haya ya mkupuo yatalipwa kwa wategemezi wa marehemu wanaotambulika kisheria kama ilivyoainishwa kwenye sheria ya Mfuko, kifungu cha 39,(1) na (2)
Nuru alitaja baadhi ya vigezo vya kunufaika na pensheni hiyo kuwa malipo hayo yatalipwa kwa wategemezi wa mstaafu wa umri, ugonjwa aliyekuwa akilipwa pensheni.
Alisema wategemezi wanaostahili kulipwa ni kwa mujibu wa sheria ya mfuko huo kifungu namba (1) na (2) mjane au mgane au watoto walio chini ya umri wa miaka 18 (miaka 21 ikiwa bado wapo shuleni).
Aliongeza kuwa mfuko huo umefanya maboresho mbalimbali ya kiutendaji ili kufanikisha malengo ya maendeleo kwa mwanachama, ikiwemo kuboresha sifa za kustahili kunufaika na huduma za mfuko.
“Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma umeboresha kiwango cha pensheni ili kuimarisha ustawi wa wastaafu wake na wanufaika wengine. Kuanzia Januari 2025, wanufaika waliopo kwenye daftari la pensheni watapata nyongeza ya asilimia mbili kwenye pensheni zao halisi,” alisema Mahinya.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Mara, Jacob Mugini, aliipongeza PSSF kwa kuwajengea uwezo waandishi wa habari na kuwataka waendelee kutoa elimu kwa wanahabari ili kutumia kalamu zao kuhabarisha jamii kuhusu huduma za mfuko huo.
"Mafunzo haya yamefungua fursa kubwa kwa waandishi wa habari wa Mkoa wa Mara. Ni mara ya kwanza kufanyika tangu nipokee kijiti cha uenyekiti wa klabu hii. Naomba semina kama hizi ziwe endelevu na zizae matunda, huku zikiwa chachu ya maendeleo,” alisema Mugini.
Naye Afisa Uhusiano Mkuu wa PSSF kutoka Makao Makuu Dodoma, Rehema Mkamba, alisema mafunzo hayo yameshatolewa pia katika mikoa ya Tabora, Morogoro, Ruvuma, Kigoma pamoja na Visiwani Zanzibar.
Alisema matarajio ya taasisi hiyo ni kuona waandishi wa habari wakifikisha elimu hiyo kwa walengwa ili kusaidia kutatua changamoto na maswali mbalimbali yanayowakabili wanachama wa PSSF.
"Tunaamini wanahabari hawa wataisaidia PSSF kwa kuelimisha wananchi kuhusu huduma tunazotoa. Mafunzo haya ni endelevu na tunaahidi kuendelea kuyatoa pamoja na kurudi tena hapa Mara,” alisema Mkamba.










Comments
Post a Comment