📍 Aishukuru Kamati Kuu ya Halmashauri ya Kuu ya CCM Taifa kwa kumteua kuwa mgombea
Na Mwandishi Wetu, Korogwe
MGOMBEA wa kiti cha ubunge Jimbo la Korogwe Mjini kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), CPA Charles Njama amesema dhamana aliyopewa kupeperusha bendera ya chama hicho kwenye kinyang'anyiro cha ubunge, ni deni kubwa kwake la kuleta maendeleo mjini Korogwe.
Akizungumza tarehe 26/8 katika ofisi za chama hicho zilizopo eneo la Majengo mjini hapa mara baada ya kukabidhiwa fomu ya kugombea ubunge na msimamizi wa uchaguzi Elinlaa Kivaya, Njama alisema anaishukuru Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM kwa kumuamini na kurejesha jina lake ili agombee ubunge katika Jimbo hilo.
"Naishukuru Kamati Kuu, Kamati ya Siasa mkoa, Kamati ya Siasa wilaya na wajumbe walionichagua, kwa kujenga imani na Mimi kati ya wenzangu Saba kupeperusha bendera ya chama, Mimi siyo mshindi kilichoshinda ni chama," alisema.
Njama alisema imani aliyopewa na chama ni deni kubwa ambalo lipo moyoni mwake katika safari ya kuijenga Korogwe mpya.
Alisema anaomba ushirikiano wa wana-CCM na wananchi wa Korogwe ili kumrahisishia kazi yake ya Ubunge wakimtanguliza Mungu ili kuibadilisha Korogwe na kuipatia maendeleo.
"Leo siyo siku ya maneno mengi na siyo siku ya kampeni bali natoa shukrani zangu kwenu huku nikiamini tunakwenda kwenye uchaguzi tukiwa wamoja ili tukiwezeshe chama chetu kina kwenda kupata ushindi mkubwa," alisema na kuongeza,
"Tunadaiwa na chama chetu tulete ushindi mkubwa kwa Rais wetu, Mimi kama mbunge na madiwani wetu wote wa kata zetu tupate ushindi wa asilimia 95,".
Aliwasihi wagombea wenzake wavunje makundi yao ambapo hata hivyo alisema yalitumika vizuri kuufanya uchaguzi wao kuchangamka.
Alisema mchakato wa ubunge umekwisha ni vema wagombea wenzake wakavunja makundi likabaki kundi moja kubwa la CCM litakalokwenda kusaka ushindi.
Awali mwenyekiti wa CCM wa Korogwe Mjini Nyakusagila Nungu aliwapongeza wananchi wa Korogwe kujitokeza kwa wingi kumsindikiza mgombea huyo kwenda kuchukua fomu katika ofisi za tume hatua ambayo alisema wameandika historia mpya.
Alisema akiwa mmoja ya wagombea ubunge katika Jimbo hilo Sasa mchakato umekwisha na Sasa mgombea ni mmoja hivyo Wana CCM Wana kazi moja ya kuifanya CCM ishinde katika uchaguzi ujao ushindi wa kishindo.
"Ndugu zangu anayeongea hapa ni miongoni mwa wagombea Saba waliigombea Jimbo la Korogwe, mchakato wa kumpata mgombea mmoja umekwisha Sasa kazi ni moja ya kwenda kukiombea kura chama chetu ili kishinde,"alisema.
Alisema kilichoshinda ni chama Cha Mapinduzi hivyo waende kwenye uchaguzi wakiwa kifua mbele kutokana na serikali ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kuleta miradi mingi ya Elimu, maji, barabara na afya aliyoileta Korogwe hivyo wananchi wanapaswa kumchagua kwa kura nyingi.
Hadi Leo jioni wagombea waliokuwa tayari wamechukua fomu ni pamoja na Zainabu Shaban Madebe wa Chama Cha NLD, Ayuob Omary Mnguto AAFP, Josephine George DP, Aweso Mustafa Juma CUF na Amani Japhet Mollel.





