Na Ada Ouko, Musoma.
JUMLA ya mitungi ya gesi 561 pamoja na majiko yake ya sahani mbili inatarajiwa kutolewa kwa Watumishi wa Jeshi la Magereza Mkoa wa Mara.
Zoezi hilo ambalo limeanza kutekelezwa leo Julai 2, 2025 ambapo mitungi 81 na majiko yake imetolewa kwa Maafisa na Askari wa Gereza Musoma huku mitungi 480 na majiko iliyobaki itapelekwa katika Magereza 6 za mkoa huo.
"Mei 8, 2024, Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan alizindua Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia. Toka kuzinduliwa kwa mkakati huo, Serikali imefanya juhudi mbalimbali kuhakikisha Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia ili kuokoa mazingira pamoja na vifo vilivyokuwa vinatokana na matumizi ya nishati isiyokuwa safi na salama ya kupikia" Alisema Mjumbe wa Bodi ya Nishati vijijini(REB) Lucas Malunde wakati wa hafla ya ugawaji wa mitungi hiyo.
Malunde alizungumza kwa niaba ya Mwenyekiti wa Bodi hiyo Mhe, Balozi Meja Jenerali (Mstaafu) Jacob Kingu, alisema hatua hiyo ni kuunga juhudi za Raisi wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Mhe, Dkt Samia Hassan kwa kutekeleza mkakati wa Taifa wa matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa vitendo.
Anasema kuwa Mhe, Rais ameweza kutoa fedha zilizowezesha magereza zote nchini kuachana na matumizi ya kuni na kuanza kutumia nishati safi ya kupikia, na kwamba kwa mkoa wa Mara, zoezi hilo limetekelezwa katika Gereza Musoma kwa kugawa mitungi ya gesi ya kilogramu 15 sambamba na jiko la gesi la sahani mbili kwa Watumishi 81 wa gereza hilo jambo ambalo ni juhudi za Mhe. Rais katika kuhakikisha Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia unatekelezwa kwa vitendo.
Awali akitoa taarifa kuhusu mradi huo, Kaimu Meneja Usaidizi wa Kiufundi kwa Wawekezaji Miradi kutoka Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Emmanuel Yesaya amesema kuwa jumla ya mitungi ya gesi ya Kilogramu 15 na majiko ya gesi ya sahani mbili 561 itagaiwa kwa Watumishi wa Magereza Mkoa wa Mara.
Kwa upande wake Kamishna Msaidizi wa Magereza wa ACP. Hospitius Mendi Mkuu wa Magereza Mkoa wa Mara ameishukuru Serikali kupitia REB kwa kuwawezesha Watumishi wa Magereza kupata nishati safi ya kupikia na kuahidi kuwa watakuwa mabalozi kwa wengine katika kampeni hiyo.
" Jeshi la Magereza Mkoa wa Mara lina jumla ya Magereza sita na yote kwa sasa yanatumia Nishati safi katika kupikia chakula cha Mahabusu na wafungwa, Na hivi karibuni Gereza Mugumu (Tabora B ) litakuwa na chanzo nyongeza ya Nishati safi (BIOGAS)"alisema Mendi.










Comments
Post a Comment