* Asema wapewe nafasi waoneshe uwezo wao
Na Mwandishi Maalum, China
MANENO hayo yamezungumzwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayesimamia Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Ndg. Ridhiwani Kikwete alipokuwa akihutubia mkutano wa Vijana Wa Dunia katika Mji wa Suzhou, China.
Mkutano huo ambao ukutanisha vijana toka nchi mbalimbali duniani wakiwemo toka asasi za kiraia, mashirika ya kitaifa na kimataifa na serikali mbalimbali, ulibeba ujumbe unaosema Vijana ni Chachu ya Maendeleo Endelevu wapewe nafasi kuonyesha Uwepo Wao.
Mkutano huo umekamilika kwa kutengeneza maazimio ambayo kila nchi iliyoshiriki itapaswa kuyaangalia ili kunyanyua ustawi wa vijana katika kushiriki ujenzi wa mataifa.
Mkutano huo ambao ulilenga pia kuangalia mafanikio katika utekelezaji wa Malengo ya Millenia kwa upande wa vijana ulihudhuria na kuhutubia kwa njia ya mtandao moja kwa moja na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Kazi Duniani (ILO) Gilbert Houngbo na Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa-UNFPA Nchini China Nadia Rasheed.
Audha mkutano huo kwa pamoja walitoa msukumo kwa serikali na wadau wa maendeleo kuhakikisha wanatoa nafasi za kuwasikiliza na kuwahamasisha vijana kushiriki katika ujenzi wa sekta za maendeleo na kuwa wamoja katika kuyafikia malengo yao pamoja na yale yanayowawezesha kuendelea.
Akihutubia Mkutano huo, Waziri Kikwete ameweka wazi hatua mbalimbali ambazo zimefikiwa na serikali ya Awamu ya Sita ya Tanzania chini ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan katika kuwawezesha vijana ikiwemo msisitizo mkubwa uliowekwa Kisera, kisheria na mipango mbalimbali ya kimaendeleo.
Pia Waziri huyu wa Vijana alieleza na kuchambua vizuri hatua mbalimbali za mipango ya maendeleo na ushiriki wa vijana ikiwemo ile ya mgawanyo wa Asilimia 10 za mapato ya ndani ya Halmashauri.
Pia alitaja Asilimia 30 za fedha za manunuzi ya umma, mikopo ya uwezeshaji wa Umma ikiwemo ya NEEC, BEST na hatua ya kushusha riba kwa wakopaji katika mabenki ya biashara, uundaji wa Sera mpya ya Vijana nchini.
Programu za maendeleo kama BBT-Madini, Kilimo, Mifugo ambazo zimeonyesha mafanikio makubwa kwa Sasa nchini baada ya utekelezaji kwa vijana.
Mkutano huo uliomalizika kwa mafanikio makubwa unakuwa ni mkutano wa 14 kukutanisha nchi wanachama na unafungua fursa kwa nchi wanachama , kukutana na kupeana uzoefu katika kushughulikia changamoto mbalimbali zinazowakabili vijana Duniani.