MKUU wa mkoa wa Mara Mhe, Kanali Evans Mtambi leo Julai 3, 2025 amewaapisha Wakuu wapya wa Wilaya za Butiama na Serengeti na kuwaelekeza, kuzingatia vipaumbele vya miradi ya maendeleo ya mkoa huo.
Rc Mtambi amebainisha vipaumbele hivyo kuwa ni pamoja na usimamizi mzuri wa mchakato wa uchaguzi katika maeneo yao ili ufanyika kwa usalama, pia kusimamia kikamilifu utekelezaji wa mikakati ya utoaji chakula kwa wanafunzi shuleni ili kuwawezesha usikivu wawapo darasani na kuinua ufaulu.
"Kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa kutokana na fedha zinazotolewa na Serikali ya Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hakikisheni miradi inatekelezwa kwa wakati kwa kuzingatia ubora na thamani ya fedha" Amesema Mtambi.
Aidha amewataka kutenga muda maalumu wa kushughulikia migogoro, kero na malalamiko ya wananchi hususani migogoro ya ardhi ambayo imekuwa ikiongezeka kwa kasi.
Alisema utatuzi wa migogoro hiyo utasaidia kuongeza utulivu katika jamii na kuwezesha wananchi kutumia muda mwingi katika shughuli za kiuchumi.
Pia amewataka kuzisimamia kikamilifu Halmashauri katika ukusanyaji wa mapato na kubuni vyanzo vipya ili kuziwezesha kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.
"Chukueni hatua kali dhidi ya watendaji watakaobainika kujihusisha na ubadhirifu wa mapato ya serikali"Ameongeza kusema.
Sambamba na hayo amewataka kufanya maandalizi ya mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa utakaopokelewa mkoani Mara Agosti 15, 2025 kwa kujiridhisha juu ya viwango stahiki vya utekelezaji miradi itakayokaguliwa.
Mara baada ya kuapishwa Mkuu wa Wilaya ya Serengeti Angelina Lubella alitoa shukrani kwa kuheshimishwa na Rais Samia Hassan na Mkuu wa mkoa wa Mara ambapo aliahidi kufanya kazi kwa bidii, uaminifu, uadilifu na kwa ushirikiano viongozi wenzake waliopo katika wilaya hiyo.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Butiama Thekla Mkuchika aliishukuru serikali kwa kumuamini na kumpa nafasi hiyo na kuahidi kutekeleza majukumu yote waliyokabidhiwa kwa kuzingatia haki na uadilifu ili wilaya hiyo iendelee kuwa salama na iwe kivutio kwa watalii.









Comments
Post a Comment