Na Ada Ouko, GMTV, Musoma.
JAMII imetakiwa kuacha kununua dawa za binadamu na kuzitumia kiholela bila kuzingatia matumizi sahihi ya dawa hizo kutoka kwa wataalamu, kwa kuwa hali hiyo inapelekea usugu wa vimelea vya magonjwa.
Mwito huo umetolewa Julai 11, 2025 na Mfamasia mkuu wa Mkoa wa Mara Apolinary Mwakabala wakati akihitimisha mafunzo ya siku mbili kwa watoa huduma za dawa kwenye maduka ya dawa muhimu (ADO) ikiwa lengo ni kupunguza usugu wa vimelea kwenye dawa aina za Antibiotic, na dawa za kuzuia maumivu kwa mtumiaji.
"Acheni kuuza dawa kiholela mgonjwa akifika dukani kwako kupata dawa kama anaumwa mnapaswa kumshauri kwenda kupima zahanati au Hospitali kwanza...
Ili kubaini ugonjwa unaomsumbua ndipo utaweza kumpa dozi kamili ya dawa kama alivyoandikiwa na daktari, badala ya kumpa dozi nusu jambo ambalo ni hatari kwa afya yake"Anasema Apolinary.
Aidha amewataka kuzingatia sheria kanuni, taratibu za uendeshaji wa huduma za maduka ya dawa muhimu (DLDM) sambamba na hilo kuacha kutekeleza huduma za kitababu na kwamba atakayebainika kufanya hivyo hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.
Mariamu Daudi ni miongoni mwa watoa huduma za dawa hizo na mshiriki wa mafunzo hayo anafurahia kupata na kusema kabla ya kupata elimu juu ya matumizi sahihi ya dawa hizo alikuwa anauuza dawa kulingana na matakwa ya wateja wake bila kubaini kuwa ni kosa.
"Mgonjwa alikuwa akija kupata dawa akiomba vidonge viwili, au vitatu nampa kumbe ni kosa akitaka Amoxlyne nusu namuuzia hama Panado tano, au hata mseto nusu nilikuwa natoa kumbe mgonjwa akitumia dawa namna hiyo inasababisha usugu wa vimelea vya ugonjwa na dawa inashindwa kumponesha kabisa" anaeleza Mariamu.
Anasema wakufunzi wa mafunzo hayo wamewataka kutoa elimu kwa jamii juu ya matumizi sahihi ya dawa kwa kunywa dozi nzima pia kuhakikisha wanatembelea vituo vya afya na hospitali kufanya vipimo kabla hawajanunua dawa hizo ili kuboresha afya zao.
Frank David mshiriki wa mafunzo hayo na ni mtoa huduma za dawa kutoka wilaya ya Bunda anasema kuwa usugu wa dawa unasababisha kuzalishwa kwa magonjwa sugu yasiyoambukiza kama vile, Kisukari, Kansa na hata Shinikizo la damu aina zote,
Jumla ya watoa huduma za dawa wapatao 450 kutoka katika halmashauri sita za wilaya za Musoma, Serengeti Butiama,Bunda na Tarime na Rorya mkoani Mara wamefanikiwa kushiriki mafunzo hayo yaliyofanyika Julai 10 na Julai 11, 2025 ambayo yaliyoandaliwa na Baraza la Famasi kwa kushirikiana na Taasisi ya Serikali( TAESCO) na chama cha wafamasia nchini.
Mwisho.







Comments
Post a Comment