Na Mwandishi Wetu - Rufiji
Waumini wa dini ya kiislam wilayani Rufiji wamefanya dua maalum ya kumwombea Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan na amani ya Tanzania kwa ajili ya maendeleo na ustawi wa wananchi kwa ujumla.
Mwenyekiti wa Baraza la waislam Tanzania Wilaya ya Rufiji Shehe Ally Mbwana amesema katika kuadhimisha sikukuu ya Idd leo Juni, 7, 2025 waislam wa Rufiji wameamua kumwombea Mhe.Rais Samia na Tanzania ili nchi iwe na amani na kuwa na mafanikio.
"Ndugu zangu leo tunakwenda kuliombea taifa letu liendelee kuwa na amani pia kumwombea Mhe. Rais wetu ili Mwenyezi Mungu amwezeshe aendelee kuliongoza vema taifa letu." Amesema Shehe Mbwana.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais -TAMISEMI, Mhe. Mohamed Mchengerwa ambaye pia ameshiriki kwenye dua hiyo amefafanua kuwa Tanzania imebarikiwa kuwa na amani hivyo ni muhimu kuilinda amani hiyo kwa faida ya vizazi vya sasa na baadaye
" Watanzania wenzangu,wa dini zote ni muhimu tukatambua maendeleo tuliyonayo sasa chini ya uongozi thabiti wa Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan yanatokana na amani ambayo imejengwa na viongozi wetu kuanzia enzi za baba wa taifa, mwalimu Nyerere hivyo tusije tukathubutu kuichezea" amesisitiza Mhe. Mchengerwa
Amesisitiza kuwa amani inapovunjika familia hazikai pamoja, akina mama, watoto na wazee ndiyo wanaoongoza kwa kuteseka hivyo ni muhimu kuilinda amani ya nchi yetu kwa kuwa hatuna Tanzania nyingine.
Amemshukuru Mhe Rais kwa kutoa fedha kwa ajili ya miradi mbalimbali ya elimu, afya na miundombinu kwenye Halmashauri zote nchini ambapo amesema sekta hizo kwa sasa zimeboreshwa kuliko awali katika kipindi kifupi cha Rais Samia.
Akitolea mifano ya kuboreka kwa sekta hizo, Mhe. Mchengerwa amesema kumekuwa na ongezeko kubwa la vituo vya afya, shule za Msingi na Sekondari katika jimbo la Rufiji.
Dua hiyo maalum ya kumwombea taifa la Tanzania na Mhe. Rais na Serikali yake imefanyka kwenye Msikiti wa Masjid Jumuiyya katika Mji wa Ikwiriri- Rufiji.