📍Asema anaheshimu mchango aliopewa na vijana kwa ajili ya fomu
📍 UVCCM wampa fedha za kuchukua fomu, wamuahidi kumuunga mkono
Na Mwandishi Wetu, Muheza
NAIBU Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Hamisi Mwinjuma maarufu MwanaFA awewataka vijana kuwa makini katika upigaji wa kura za maoni ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kuhakikisha wanachagua wagombea wenye kesho nyingi kwa ajili ya kusaidia kuleta maendeleo wilayani Muheza.
Akizungumza kwenye Kambi ya vijana iliyofanyika shule ya sekondari Chief Mang'enya, MwanaFA ambaye pia ni mbunge wa Muheza alisema kuelekea upigaji wa kura za maoni ni vizuri vijana wakawaunga mkono wagombea wataoivusha CCM katika uchaguzi Mkuu wa Oktoba.
"Kundi hili kama Kila kitu kitakaa sawa na rehema ya mungu, lina kesho nyingi kuliko jana, linatakiwa kuunga mkono vijana wenzao wenye kesho nyingi kuliko kuunga mkono wenye jana nyingi kuliko kesho chache na wana jana nyingi ambazo hawakujali mambo yetu," alisema.
Alisema amefurahi kuwaona vijana wanasema na kutaja miradi ambayo imetekelezwa na serikali ya awamu ya sita chini ya Rais wetu mpendwa Dkt Samia Suluhu Hassan na hivyo hawawezi kuhadaika na maneno ya wapinzani.
Alisema kama vijana wanajua kilichofanywa na viongozi wao, chama chao na serikali yao hawawezi kuhadaika kwakuwa kundi la vijana ndilo ndiyo rahisi kuhadaika na kutumika vibaya kisiasa.
Alisema katika miaka mitano, vijana wengi waliokuwa kwenye uongozi wamefanya mambo makubwa yasiyomithirika kuliko wakati wowote ule tangu wilaya hiyo ilipoasisiwa mwaka 1974.
"Mimi wakati mwingine nimekuwa nikiwaheshimu wazee wetu waliopita kabla yangu lakini kibinadamu ukilinganisha kazi zilizofanyika, sisi tumefanya vizuri zaidi yao na hata katika mahusiano," Alisema na kuongeza,
"Miaka mitano hii mmenipa ushirikiano usiomithirika, sina maneno mazuri ya kuwashukuru namna moyo wangu ulivyofurahi kiukweli nawashukuru sana na najua mtalinda kura zangu,".
MwanaFA aliwashukuru vijana kwa mchango wao wa fomu na amewaahidi atawaunga mkono baadhi yao ambao watagombea udiwani ili kuendelea kuonesha umoja na kuijenga Muheza.
Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM wilaya ya Muheza (UVCCM) Aziza Mshakangoto alimshukuru mbunge kwa niaba ya Umoja huo kwa kufanya shughuli mbalimbali ambazo aliziunga mkono na kufanya kazi za UVCCM wilayani humo kufanyika kwa ufanisi mkubwa.
Alisema kutokana mambo mbalimbali ambayo mbunge huyo ameyasimamia na kukipa heshima chama cha Mapinduzi wao kama vijana hawana budi kumuunga mkono katika dhamira yake ya kugombea tena Jimbo hilo.
"UVCCM tutakuunga mkono katika dhamira yako ya kuendelea kuwatumikia watu wa Muheza kwa maana umefanya kazi yetu katika jumuiya iwe nyepesi lakini pia ilani yetu ya CCM imetekelezwa kwa kiasi kikubwa," alisema Aziza.
Makatibu wa UVCCM wa kata zilizo katika tarafa nne za Muheza, Bwembwera, Lusanga na Ngomeni wote walionesha hisia zao za kumuunga mkono MwanaFA kwa kuwa amefanya kazi ambazo zimewakosha.
Awali Katibu wa UVCCM wilaya ya Muheza Ajuaye Msigala alisema Kambi hiyo ilianza Juni 18 mwaka huu na inamalizika leo Juni 24 kwa vijana zaidi ya 400 kupata mada 30 ambazo zimefundishwa na wakufunzi 20 ikiwemo wa kutoka Chuo cha CCM Ihemi Iringa pamoja na waliotoka Makamo makuu ya Chama Dodoma na kuwafanya vijana hao waive na kuwa tayari kwa uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu.








Comments
Post a Comment