#Awataka kukamilisha kazi kwa wakati
Dar es Salaam
Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Mhandisi Victor Seff amewataka makandarasi wanaotekeleza kazi za ukarabati na matengenezo ya barabara vivuko na madaraja katika maeneo yaliyoharibiwa na mvua za El nino nchini kutekeleza mikataba yao kwa wakati huku wakizingatia masuala ya msingi ikiwemo usalama mahali pa kazi pamoja na utunzaji wa mazingira.
Mhandisi Seff ameyasema hayo wakati wa kikao kilichofanyika jijini Dar es Salaam kati ya TARURA na Makandarasi hao wanaotekeleza miradi hiyo nchi nzima.
“Hakikisheni katika utekelezaji wa miradi yote mnakamilisha kwa wakati pia mnazingatia masuala yote ya usalama na mazingira kama ilivyoainishwa kwenye makubaliano ya jumla ya miradi hii”Alisisitiza.
Naye, Mratibu wa miradi ya Benki ya Dunia kutoka TARURA Mhandisi Humphrey Kanyenye amesema kwamba wao kama waratibu wa miradi hiyo wapo tayari kuhakikisha wanatoa ushirikiano wa kutosha kuhakikisha kila mkandarasi anatekeleza majukumu yake kwa ufanisi ikiwemo utunzaji wa mazingira ili kuepuka kwenda kinyume na matakwa ya utekelezaji wa miradi ya benki ya dunia.
Wakati huohuo Meneja wa TARURA Mkoa wa Dar es Salaam Mhandisi Geofrey Mkinga amewahakikishia ushirikiano makandarasi kuhakikisha wanakimbizana na muda na kukamilisha miradi hiyo yenye tija kwa mkoa wake pamoja na nchi nzima kwa wakati kwani Dar es Salaam ni moja ya mkoa wenye miradi hiyo ya dharura.
Aidha, katika kikao hicho makandarasi walipata nafasi ya kuuliza maswali mbalimbali kwa uelewa zaidi kabla ya kuanza utekelezaji wa kazi ambapo walijibiwa na kuhakikishiwa kuwa TARURA kwa niaba ya Katibu Mkuu OR TAMISEMI itahakikisha hakuna mkwamo wowote kwani dhamira ya Serikali ni kuona miradi inakamilika kwa wakati kama ilivyopangwa.
Miradi ya SERC inatekelezwa ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa mradi wa DMDP II ambapo mtekelezaji mkuu ni Katibu Mkuu OR-TAMISEMI ambapo amekasimu utekelezaji huo kwa Mtendaji Mkuu TARURA.