Na Mwandishi Wetu
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhandisi Hamad Masauni amewataka watanzania kutochukulia poa suala la utunzaji wa Mazingira badala yake wayatunze ili Tanzania iendelee kuwa sehemu salama.
Waziri Masauni aliyasema hayo jana alipokuwa akizungumza na Menejimenti ya Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kwenye Kikao Kazi kilichofanyika jijini Dodoma kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi za Baraza.
Masauni alisema katika kuhakikisha suala la utunzaji wa mazingira linakuwa endelevu Baraza linatakiwa kuwekeza nguvu zaidi katika eneo la utoaji wa huduma na elimu kwa umma.
Alisema NEC ikifanya hivyo itasaidia watanzania waielewe Sheria ya Usimamizi wa Mazingira na kuona wana wajibu wa kuyatunza Mazingira.
Alisema Baraza lina jukumu kubwa la kuhakikisha mazingira yanatunzwa na ili suala hilo lifanikiwe ni lazima kila mmoja kutimiza majukumu yake katika uhifadhi na usimamizi wa mazingira.
Aidha, Waziri aliwataka wahamasishe elimu kwa umma kuhusu umuhimu wa kuhifadhi mazingira kwani wananchi bado hawana elimu ya kutosha kuhusu umuhimu wa kuhifadhi mazingira.
Alisema kwa wananchi kukosa elimu ya mazingira kumechangia washiriki katika shughuli zinazochangia uharibifu wa mazingira kama ukataji miti hovyo, uchomaji misitu na utupaji taka ovyo.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Baraza, Dk Immaculate Semesi alimpongeza Waziri kwa kutoa nafasi ya kukutana na Menejimenti ya Baraza na kupokea maoni mbalimbali yaliyotolewa kwa ustawi wa Baraza na Taifa kwa ujumla.






Comments
Post a Comment