Tarime, Juni 28, 2025 Katika hali ya kusisimua na ya kipekee kabisa, Mzee Geregole Mgendi Nyanchini mwenye umri wa miaka 85 ameandika historia mpya leo baada ya kuchukua rasmi fomu ya kuwania ubunge wa Jimbo la Tarime Mjini kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Mzee Nyanchini, ambaye ni mkazi wa muda mrefu wa Tarime na mkongwe aliyejikita katika siasa na maendeleo ya jamii, amesema ameamua kujitosa katika kinyang’anyiro hicho kwa lengo la kutumia busara na uzoefu wake katika kuwahudumia wananchi kwa haki, heshima na maadili ya uongozi wa kizalendo.
“Nimeamua kuchukua fomu kwa sababu naamini bado nina uwezo wa kulisemea jimbo hili, kulitumikia kwa moyo mmoja, na kuhakikisha kila mwananchi anapata haki yake ya msingi ya maendeleo,” amesema Mzee Nyanchini akiwa amevalia sare ya kijani ya chama chake.
Hatua yake hiyo imeibua hisia mseto kwa wakazi wa Tarime Mjini, wengi wakimtazama kama mfano wa uzalendo na dhamira ya kweli ya kulitumikia taifa bila kujali umri. Wengine wameonyesha kuvutiwa na uthubutu wake, wakisema kuwa ni alama ya matumaini na mshikamano wa vizazi tofauti katika kujenga mustakabali bora wa Tarime.
“Huu ni uthibitisho kuwa mapenzi ya kweli kwa nchi hayaangalii umri. Tunamheshimu sana Mzee Nyanchini kwa uamuzi wake huu wa kishujaa,” alisema mmoja wa vijana waliomshuhudia akichukua fomu.
Mzee Geregole pia amewaasa vijana kujitokeza kwa wingi kuchukua fomu na kushiriki kikamilifu katika mchakato wa uchaguzi, akisema demokrasia imara hujengwa kwa ushiriki mpana na wa hiyari wa wananchi wote.
Mchakato wa uchukuaji fomu za kuwania nafasi mbalimbali za uongozi kupitia CCM umeendelea kwa kasi wilayani Tarime huku wanachama wa kada mbalimbali wakijitokeza kwa nia ya kuwatumikia wananchi.




Comments
Post a Comment