Waziri wa Nchi ofisi ya Waziri Mkuu,Kazi,ajira,Vijana na Wenye ulemavu Ridhiwani Kikwete amekutana na kufanya mazungumzo na ujumbe wa Ubalozi wa Jamhuri ya Watu wa China ukiongozwa na Balozi wa China Nchini Balozi Chen Mingjian Ofisini, Dodoma.
Balozi Mingjian alitumia kikao hicho kujitambulisha na kuendelea kuimarisha mahusiano baina ya nchi ya China na Tanzania.
Aidha alikumbusha maeneo muhimu ya ushirikiano haswa katika mafunzo ya kujenga ujuzi na ufundi huku msisitizo mkubwa ukiwa kuwaandaa vijana watakaopambana na mabadiliko makubwa ya kidunia hasa katika mapinduzi ya Teknolojia.
Kwa upande wake, Waziri Kikwete amemuhakikishia Balozi Mingjian na Ujumbe wake kuwa Tanzania itaendelea kuenzi uhusiano uliopo baina yake na China sanjari na kuendeleza uhusiano huo kwa kuimarisha maeneo yote ya mashirikiano hayo.
Pia Waziri Kikwete ameishukuru serikali ya China kwa mabadiliko makubwa ambayo yanaelekea kukuza ujuzi kwa vijana wa Kitanzania na nia yao ya kufanya maonyesho makubwa ya Kazi yanayolenga kufunua fursa za vijana wa kitanzania kujiajiri pamoja na kufungua milango ya kuajiriwa na makampuni makubwa ya kigeni yakiwemo ya China nchini hapa.