▪️Vijana kupatiwa fursa ya kupata vifaa vya pikipiki na Bajaj kwa unafuu
▪️Vijana zaidi ya 2000 kunufaika na awamu ya kwanza ya Progamu
▪️RC Senyamule awataka kuzingatia sheria ili kupunguza ajali
▪️Mbunge Mavunde awawezesha kufungua SACCOS
Dodoma
Wasafirishaji abiria kupitia pikipiki na Bajaj Jijini Dodoma wanategemea kunufaika na programu ya 𝙂𝙪𝙧𝙪𝙙𝙪𝙢𝙪 𝙡𝙖 𝙈𝙖𝙢𝙖 inayoratibiwa na kampuni ya RoadMaster kwa lengo la kusaidi upatikanaji wa matairi mapya kwa Bajaj na Bodaboda katika mfumo rahisi ambao utawawezesha kundi hili kubwa la wasafirishaji kupata vitendea kazi kwa urahisi na kwa muda mfupi.
Hayo yamesemwa jana Jijini Dodoma wakati wa uzinduzi wa Programu ya 𝙂𝙪𝙧𝙪𝙙𝙪𝙢𝙪 𝙡𝙖 𝙈𝙖𝙢𝙖 iliyozinduliwa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mh. Rosemary Senyamule.
Akitoa maelezo ya programu,Mkurugenzi wa RoadMaster na Mratibu wa Progamu hii Ndg. Thuwein Makamba amesema lengo kubwa la programu hii ni kuwawezesha wasafirishaji kuwa na matairi yenye ubora ili kusaidia kupunguza ajali zisizo za lazima ambazo husababishwa na uchakavu wa matairi.
“Najua wasafirishaji wengi wanakumbwa na changamoto ya upatikanaji wa matairi bora kwa wakati kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo gharama kuwa juu.
Programu hii itampatia kijana tairi linalouzwa Tsh 70,000 kwa malipo ya awali ya Tsh 10,000 tu na baadaye atalipia kwa kila siku Tsh 1800 kwa kipindi cha mwezi mmoja.
Lengo ni kuhakikisha anapata kwanza usalama wa chombo chake kabla ya kuhangaika na kupata fedha iliyo kamili kwa wakati mmoja ili kununua tairi.
Hii programu inaunga mkono kazi kubwa anayofanya Mh. Rais Dkt. SamiaS. Hassan katika kuwajali waendesha pikipiki na Bajaj nchini”Alisema Thuwein
Naye Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mh. Rosemary Senyamule amepongeza hatua hii ya urahisi wa upatikanaji wa matairi kwa vijana na kuwataka wasafirishaji hao kuzingatia sheria ili kupunguza ajali zisizo za lazima zinazosababishwa na uzembe au kutozingatia sheria.
Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini Mh. Anthony Mavunde amepongeza programu hiyo yenye lengo la kuwapa urahisi vijana kupata tairi zenye ubora kwa gharama nafuu na kutumia fursa hiyo kuwataka vijana ambao amewasaidia kuanzisha SACCOS kuchangamkia fursa ya mkopo ya asilimia 10 ya Jiji ili kila mmoja amiliki chombo chake kwa kuwa Jiji limetenga Bilioni 7 kukopesha wanawake,Vijana na watu wenye ulemavu.
Naye Mwenyekiti wa Umoja wa Waendesha Pikipiki na Bajaj Dodoma(UMAPIDO) Ndg. Marwa Chacha Nyagate amemshukuru Mh. Rais Dkt. Samia S. Hassan kwa kuendelea kuyajali makundi maalum katika jamii na kuahidi kuichangamkia fursa hii ya upatikanaji wa tairi hizi zenye ubora mkubwa ambazo mfumo wa upatikanaji wake ni rahisi na rafiki kwa vijana wengi ambao vipato vyao ni vidogo.









Comments
Post a Comment