Na Mashaka Mhando, Tanga
KUFUATIA kuboreshwa kwa bandari ya Tanga, Kampuni ya Simba Logistics ya Jijini Dar es Salaam, wamemshukuru Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kufanya maboresho hayo ambayo yamesaidia kampuni hiyo kuajiri vijana 300.
Akizungumza katika sherehe za siku ya mazingira zilizofanyika katika shule ya sekondari Ummy Mwalimu iliyopo kata ya Maweni, Meneja Utekelezaji wa Simba Logistics Daud Kanuti alisema wanaishukuru serikali kupanua bandari hiyo ambayo imeanza kuleta manufaa.
"Mheshimiwa mkuu wa mkoa tunaomba utufikishie salamu zetu kwa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa maboresho aliyofanya bandari ya Tanga, imesaidia kuongoza ajira, vijana 300 wa Kitanga tumewapa ajira ya muda mrefu na muda mfupi, tunaishukuru sana serikali," alisema.
Kanuti alisema kuwa kampuni hiyo iliyoanza kazi katika Jiji la Tanga mwaka 2019 baada ya maboresho hayo, tayari wameleta meli 10 ambazo zimekuja na bidhaa mbalimbali.
Kuhusu suala la mazingira Kanuti alisema kampuni hiyo inaunga mkono suala hilo la imetoa miche 10,000 ya minazi kwa ajili ya kupandwa katika maeneo ambayo mkoa itachagua.
"Mkuu wa mkoa kampuni yetu inatoa miche 10,000 ya minazi ili kuunga mkono juhudi za utunzaji na uhifadhi wa mazingira katika mkoa wetu," alisema Kanuti na kuongeza kwamba mwaka jana walitoa miche 12,000.
Akizungumza katika sherehe hizo, Mkuu wa mkoa wa Tanga Balozi Dkt Batilda Salha Buriani, aliwapongeza wadau wa mazingira kwa kusaidia kampeni ya upandaji miti mkoani humo.
Aliishukuru kampuni ya Simba Logistics kwa kutoa miche ya minazi akieleza kwamba mkoa wa Tanga una kila sababu ya kurejesha zao na nazi ambalo huko nyuma lilikuwa likilimwa kwa wingi.
Alisema wazee wa zamani wa Tanga waliweza kupanda miti mingi ya minazi lakini Sasa mkoa huo kama vile zao hilo lonatoweka taratibu.
"Tunawashukuru Simba Logistics kwa miche hii, kama mkoa tunataka kurejesha zao la minazi ili kizazi kijacho kisituhukumu kwamba hatupanda minazi tulikula ya mababu zetu sisi tukaacha," alisema na kuongeza,
"Miti tutakayopanda itazamwe isiachwe ikakauka, tuimwagilie maji ili ikue kama lengo letu tulivyokusudia," alisema.
Naye Ofisa Mawasiliano wa taasisi ya Forest Focus Hilda Mollel alisema taasisi yao inatoa miti ya asili kwa asilimia 75 na miti ya matunda kwa asilimia 25 bure kwa taasisi zinazojihusisha na uhifadhi wa mazingira.
Alisema wanaunga mkono juhudi za Rais Dkt Samia Suluhu Hassan za uhifadhi wa mazingira kwa kutoa elimu kwa wananchi juu ya suala la utunzaji na uhifadhi wa mazingira.
Mwakilishi wa taasisi ya uhifadhi ya Mwambao Ahmad Salim inayojihusisha na uhifadhi wa bahari katika mkoa ya Tanga na Zanzibar, hivi karibuni watapanda mikoko kwa wastani wa hekta 10,000.



.jpg)
.jpg)

.jpg)
Comments
Post a Comment