📍JIMBONI BUTIAMA
Wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tawi la Kitaramanka wameungana na wananchi wengine kumuweka rasmi Mbunge wa Jimbo la Butiama na Naibu Waziri Katiba na Sheria Mhe. Jumanne Sagini katika maombi ya kila siku mpaka atakapopitishwa kwenye uchaguzi ujao baada ya kuwakamilishia ujenzi wa Ofisi ya Chama.
Wakizungumza katika hafla fupi ya makabidhiano ya bando za bati kutoka kwa Watumishi Ofisi ya Mbunge Afisa Mahusiano Ndg. Japhet Changarawe na Katibu Ndg. Samson Malima wamesema kuwa Mbunge Sagini aliwahidi kuwachangia kiasi katika ujenzi lakini amefanya zaidi kwani amejenga na kukamilisha ofisi hivyo tayari wamemthibitisha kumuombea mema kila siku ili azidi kuendelea kuiongoza Butiama.
"Kwa maendeleo na mambo mema aliyotufanyia Mbunge Sagini Wanachama wote tulikaa kikao cha kumuweka katika maombi ya kila siku ili Mwenyezi Mungu amuongezee pale alipotoa pia amjalie afya njema na katika uchaguzi wa mwaka huu apite kwa kishindo maana tunaimani naye na hatuko tayari kumuacha kiongozi muadilifu kama huyu," amesema Mseti Nyansambo Makori Katibu wa CCM Tawi la Kitaramanka.
Kwa upande wake Mwenyekiti Kijiji cha Kitaramanka Mhe. Cartstus Patrick ameeleza kuwa Mbunge Sagini amekuwa ni wa vitendo maendeleo mengi kayafanya katika Kijiji cha Kitaramanka ambapo amegusa taasisi binafsi na za serekali pia na jimbo lote kwa ujumla amelitendea haki hivyo hana budi kumuombea kila siku.
Aidha, Afisa Mahusiano kutoka Ofisi ya Mbunge Jimbo la Butiama amewaomba wanachama hao kuendelea kumuunga mkono Mbunge Mhe. Jumanne Sagini ambapo amesema kuwa maendeleo yaliyofanyika Kijiji cha Kitaramanka yamefanyika vijiji vyote 59 vya Wilaya ya Butiama.



Comments
Post a Comment