Na Shomari Binda-Musoma
MKUU wa mkoa wa Mara Kanali Evans Mtambi ameanika mafanikio lukuki ya Utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ( CCM) katika kipindi cha mwaka 2020/2025.
Mafanikio hayo ni katika sekta ya afya,elimu,maji,umeme,miundombinu na huduma za jamii ambayo imetokana na serikali ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kupeleka fedha nyingi za miradi kwenye mkoa huo.
Akisoma taarifa ya utelezaji huo kwa wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Mkoa ya CCM leo mei 22,2025.katika hutuba iliyochukua zaidi ya saa 2 amesema wana CCM wanapaswa kutembea kifua mbele na mafanikio hayo.
Amesema serikali imetoa kiasi cha shilingi tilioni 6.8 ambazo zimetekeleza miradi ambayo imekuwa na manufaa kwa wananchi.
Mtambi amesema miradi ya elimu ikiwemo ujenzi wa shule mpya na madarasa yamejengwa pasipo kuwachangiaha wananchi na kuwezesha wanafunzi kusoma maeneo sahihi.
Amesema kwenye eneo hilo la elimu utekelezaji mkubwa umefanywa na kutoa shukrani kwa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan wa miradi hiyo.
Sekta ya afya amesema utekelezaji unaonekana kwa kila mmoja kuanzia ujenzi wa zahanati vituo vya afya na hospital vikiendana na kuwekwa vifaa tiba na upatikanaji wa dawa.
Amesema wananchi wamekuwa wakipata huduma bora za afya na kwa sasa kwa mkoa wa Mara umekuwa ukipokea watalii wa huduma ya afya kutoka nje ya nchi kupitia hospital ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere na kuhudumiwa.
Kwenye huduma za maji
Mkuu huyo wa mkoa amesema Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan amemtua mwanamke ndoo kichwani kupitia RUWASA na MUWASA kwa kutekelezwa miradi mingi ya maji.
Amesema kwenye Vijiji RUWASA imefanya kazi kubwa ya kuwafikishia wananchi huduma huku MUWASA kupitia miradi yake hususani kwa manispaa ya Musoma imewafikia wananchi kwa zaidi ya asilimia 98.
" Ndugu zangu Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan amefanya kazi kubwa ambayo tukiongea hapa kila kitu muda hautatosha na nimeona wajumbe wanasinzia na wengine wanatoka nje.
" Yapo mambo makubwa yamefanyika kwenye sekta ya kilimo na elimu imekuwa ikitolewa kwa wakulima wetu ili wafanye kilimo chenye tija",amesema.
Katika kuwawezesha wananchi kiuchumi kupitia mikopo isiyo na riba ya asilimia 10 inayotolewa kwenye halmashauri jumla ya shilingi bilioni 2.93 zimetolewa kwa vikundi 324 vya wanawake,vijana na wenye ulemavu.
Mtambi amesema serikali ya mkoa wa Mara inamshukuru Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan na kuahidi kusimamia vizuri fedha zote zinazopelekwa mkoa wa Mara kwaajili ya utekelezaji wa miradi.
Awali akifungua kikao hicho Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Mara Patrick Chandi amesema kupitia Kamati ya ,Siasa ya mkoa iliyofanya ziara kwenye miradi 38 wameridhika na utekelezaji wa ilani.
Amesema kwa kazi nzuri iliyofanywa na serikali ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan wanao uhakika wa kufanya vizuri kwenye uchaguzi mkuu wa 2025.







Comments
Post a Comment