Jeshi la Polisi mkoani mwanza linamshikilia Diana Bundala kwa tuhuma za kugeuza makazi yake kuwa kanisa,kuendesha shughuli za kidini bila kuwa na usajili pamoja na kuhubiri kwa sauti ya Juu.
Kamanda wa polisi mkoa mwanza Naibu Kamishna wa Polisi Wilbroad Mutafungwa amesema kuwa Bundala Maarufu kwa Jina la Mfalme Zumaridi,Mkazi wa mtaa wa Buguku kata ya Buhongwa Jijini mwanza pia anahojiwa kuhusiana picha Mjongeo inayoendelea kusambaa kwenye mitandao ya kijamii ikimuonyesha akiwaeleza watoto kuwa yeye ndiye mungu wao.
Akizungumza na waandishi wa habari, Kamanda Mutafungwa amesema Polisi inaendelea na uchunguzi wa tuhuma zinazomkabili Mfalme Zumaridi kwa kushirikiana na Taasisi nyingine za serikali.
Aidha ameowaomba wananchi wenye Taarifa mbalimbali zinazoweza kusaidia uchunguzi wa tuhuma dhidi ya Mfalme Zumaridi kuziwasilisha Polisi.
Kwa mujibu wa Kamanda Mutafungwa,Uchunguzi huo utakapokamilika hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya mtuhumiwa.
Hii ni mara ya tatu kwa Mfalme Zumaridi kujikuta mikononi mwa dola ambapo mwaka 2019,Aliyekuwa mkuu wa wilaya nyamagana Philis Nyimbi aliamuru Kufungwa kwa kanisa lake kwa madai ya kuendesha ibada kinyume cha sheria za nchi.
Pia mwaka 2022 Mfame Zumaridi alikamatwa na Polisi kwa tuhuma za usafirishaji haramu wa binadamu 149 pamoja na kuwatumikisha watu hao.




Comments
Post a Comment