📍 Wampongeza mbunge Ummy kwa kutatua changamoto zinazowagusa
📍Wasema ni mbunge wa aina yake kutokea katika Jimbo la Tanga
📍 Mwenyewe ampongeza Rais kujenga vituo vingi vya afya
📍 Daktari wa macho asema ulaji mihogo chanzo cha tatizo la macho nchini
📍Bilal Muslim Mission wasema wamekuja kutekeleza ombi la mbunge
📍Yas wafurahia ushiriki wao kambi ya macho.
Na Mwandishi Wetu, Tanga
WANANCHI wa Jiji la Tanga, wamelazimika kutoa machozi ya furaha kufuatia Mbunge wa Jimbo la Tanga, Mhe Ummy Mwalimu maarufu Oddo Ummy, kuleta kambi ya huduma ya macho ya bure ambayo wananchi hao wamepimwa na kupata dawa, miwani pamoja na ushauri wa namna ya kuishi kuepuka magonjwa ya macho.
Wakizungumza katika kambi hiyo inayofanyika kwa siku tatu katika shule ya sekondari ya Usagara baadhi ya wananchi, walisema kuwa mbunge wa Jimbo la Tanga anajua kugusa changamoto zinazowakabili wananchi wake.
"Namshukuru sana mbunge, kiukweli amenitibu macho yangu, ni mbunge tunayetakiwa kumshikilia, anajua changamoto zetu," alisema Magreth Yohana au mama Saidi wa Kongwa Amboni.
Tumaini Maina mkazi wa Sahare ambaye ni mpuliza gunda wa African Sports 'Wana Kimanumanu', alisema anamshukuru mbunge kwa kuokoa wazee wenye mahitaji na matatizo ya macho katika Jiji la Tanga.
"Mimi nina miaka 70 sasa nina tatizo la macho muda mrefu, niliposikia Odo Ummy kaleta madaktari wa macho haraka nimekuja, nimepewa miwani mbili, kiukweli namshukuru sana mbunge, hatudai anatudai sisi wananchi wa Tanga kutokana na kazi lakini pia changamoto zetu anavyozijali," alisema.
Bibi Chichi mkazi wa Makorola alisema akiwa mwanachama wa CCM anajua mengi kuhusu wabunge waliopita tangu enzi za Balozi Madgid hadi Ummy Mwalimu.
"Ummy ni mbunge anayejali matatizo ya moja kwa moja yanayowakabili wananchi wa Tanga, hili la afya amefunika maana sisi wazee tumekumbwa na tatizo hilo na yeye ametupa tiba, sisi tutamlipa kura," alisema Bibi Chichi na kuongeza kuwa amewashuhudia wabunge wengi katika Jimbo la Tanga lakini Ummy, amewafunika wote.
Akizungumza katika kambi hiyo ambayo inatolewa na madaktari bingwa wa macho wa Bilal Muslim Mission kwa ufadhili wa mtandao wa Yas, mbunge wa Jimbo la Tanga Mhe Ummy Mwalimu aliwashukuru Bilal Muslim Mission Tanzania kwa kurejea tena Jijini Tanga baada ya kufanya hivyo mwaka 2019.
Alisema walipokuja Tanga mwaka huko waliona wagonjwa zaidi ya 5,000 na waliopata miwani walikuwa ni 3,000 na 400 walifanyiwa operesheni ya mtoto wa jicho.
"Mimi nafasi yangu kama mbunge nimewaomba waje tena Tanga, nashukuru wamekubali ombi langu wamekuja," alisema Ummy.
Alisema kuwa anamshukuru Mama Cerk, Beta Charitable Trust ya Uingereza kwa kufadhili wa madaktari wa macho na taasisi ya Yas.
"Ujumbe wangu kwa watu wa Tanga, tusitumie miwani hovyo hovyo bila kupima kwa wataalamu lakini pia wajitoe wanaposikia kuna kambi za macho au madaktari wa magonjwa mbalimbali ili waweze kuchunguzwa bure magonjwa waliyonayo," alisema.
Pia mhe Ummy alimshukuru na kumpongeza Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa namna alivyoijali sekta ya afya nchini kwa kuhakikisha vituo vingi vya afya, hospital na zahanati ambazo zimekuwa na vifaa tiba vya kutoka katika ngazi zote.
"Tunampongeza mhe Rais kiukweli ametutendea haki Jiji la Tanga na Tanzania kwa ujumla vifaa tiba vipo katika hospital na vituo vya afya vyote na wananchi wanapata matibabu ya uhakika katika maeneo hayo," alisema Ummy na kuongeza kuwa wanachosubiri ni kumpa kura nyingi ifikapo uchaguzi Mkuu ujao.
Daktari bingwa wa macho na mratibu wa macho mkoani Tanga, Dkt Hussein Tayebji alisema tatizo la macho limekuwa likiongezeka siku hadi siku kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo pia ulaji wa mihogo.
alisema uvutaji wa sigara, unywaji wa pombe na ulaji wa mihogo umekuwa ukisababisha tatizo la macho hivyo akataka watu watazame mienendo yao ya maisha.
"Ulaji wa mihogo unasababisha kwa kiasi kikubwa ugonjwa wa macho kitaalamu tunaita Cyanide-CN-Cassava,"alisema.
Mratibu wa kambi hiyo ya Macho kutoka Bilal Muslim Mission Aziz Sharrif alisema wamelipa uzito ombi la mbunge wa Tanga kutokana na mwanzo walipokuja waliacha wagonjwa wengi wa macho.
"Tumekuja tena kutokana na ombi la mbunge na hapa Tanga kuna wagonjwa wengi hivyo tumeonelea tuje kutoa huduma hizi za bure kwa niaba ya mbunge," alisema.
Mkurugenzi wa Kanda ya Pwani yenye mikoa ya Tanga na Morogoro wa kampuni ya simu ya Yas, Abdul Ally alisema kipekee kampuni yao imefurahia kushiriki tukio hilo la kambi ya macho na wamewaalika wananchi waliokuwa wilaya za jirani kujumuika na wenzao Tanga Jiji ili kupata huduma hizo bure.
Alisema kampuni yao ya Yas inaona ufahari kuwa miongoni mwa kampuni zilizoshiriki kutoa huduma hizo kwakuwa tatizo la macho limekuwa kubwa hivyo kwa kiasi fulani madaktari wataweza kuwaona wagonjwa hao.