Msajili wa vyama vya Siasa Tanzania, Jaji Francis Mutungi amesema hata kama kauli ya ‘No reform, no Election’ haijavunji sheria ya vyama vya siasa,lakini kamwe isitumike kama kichocheo cha kuvunja sheria za nchi na katiba ya Jamhuri ya muungano wa Tanzania.
Amesema ofisi yangu inafuatia kwa karibu kauli kama hizo zinazotumiwa na baadhi ya vyama vya siasa katika kuvunja sheria na katiba ya nchi.
Jaji, Mutungi amesema hayo wakati akizungumza na George Marato Tv huku akisisitiza kuwa hakuna chama cha siasa chenye uwezo wa kuzuia uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika badae mwaka huu 2025.
Amesema katika mazungumzo yake na waandishi wahabari baada ya kushiriki warsha ya wadau wa kujadili namna ya kuzuia na kupambana na rushwa katika uchaguzi mkuu 2025,akiwaeleza wazi mazungumzo yake na vyama vya siasa ikiwemo Chadema kwamba ofisi yake hauwezi kuvumilia kauli zinazolenga kuvunja sheria za nchi.
Tangu kumalizika kwa uchaguzi wa ndani, CHADEMA wamekuwa wakieleza kuwa, bila mabadiliko katika mifumo ya uchaguzi hakutakuwa na uchaguzi mkuu mwaka 2025 na kwamba watauzuia kwa kuandamana nchi nzima kauli ambayo inapingwa na vyama vingine vya siasa ikiwemo CCM.
Msajili huyo amesema hakuna anayeweza kuzuia uchaguzi wa mwaka huu, kwakuwa kinachosemwa ni matamshi ya wanasiasa majukwaani ambayo kila chama kinaweza kuwa na maana yake.
“Hakuna awezaye kuzuia uchaguzi kwa kutamka tu kwenye majukwaa, CHADEMA hawajavunja sheria na nilipokutana nao hivi karibuni walisema hawatakuwa tayari kuvunja sheria za uchaguzi,” amesema Jaji Mutungi.
Aidha, amesema chombo kinachoweza kuzuia uchaguzi ni mahakama na hadi sasa hakuna aliyekwenda huko isipokuwa kinachoendelea ni matamshi ya midomoni mwa wanasiasa.
Amesema hajasikia kuwa CHADEMA wamekwenda mahakamani kupinga uchaguzi licha ya kuwa wanao wanasheria wanaojua utaratibu mzima wa nini kifanyike hivyo kinachoonekana ni kama wanafanya propaganda za kisiasa ambazo haziwezi kuwatia hatiani isipokuwa kama kutakuwa na maneno mengine ndani ya kauli zao.
“Mimi nitatafuta muda wa kuwaiteni kuzungumza kirefu zaidi kuhusu mambo haya, lakini kama ulivyosema mimi ndiye baba wa vyama vya siasa ni kweli, na kila chama kina haki ya kusikilizwa lakini. siyo kuvunja sheria, sisi hatutegemei kama wanaweza kuvunja sheria,” amesema.
"Pia niwaombe wadau waache kutoa matamko kwa kutetea watu wanavunja sheria za nchi kwa kujificha kwenye kichaka cha chama cha siasa,tuache vyombo vifanye kazi zake kwa uhuru"alisema Jaji Mtungi



Comments
Post a Comment