Waziri wa Afya Jenista Mhagama, amethibitisha kuwepo kwa wagonjwa wawili wa ugonjwa wa Mpox nchini baada ya uchunguzi wa kimaabara kufanyika.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na wizara ya afya Machi 10,2025 ni kuwa wagonjwa hao walitambuliwa baada ya sampuli zao kuchunguzwa katika maabara ya Taifa.
Mmoja wa wagonjwa hao ni dereva wa magari ya mizigo aliyekuwa safarini kuelekea Dar es Salaam.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa Mpox ni ugonjwa unaosababishwa na virusi vinavyopatikana kwa wanyama jamii ya nyani na huweza kuambukizwa kwa binadamu kupitia kugusana moja kwa moja na mnyama au mtu mwenye maambukizi.
Serikali imewahakikishia wananchi kuwa imejipanga kudhibiti ugonjwa huo kwa kutumia mikakati madhubuti ya ufuatiliaji, upimaji, na utoaji wa elimu ya afya
Wizara ya Afya imewasihi wananchi kuepuka kugusana na watu wenye dalili za ugonjwa huo, kunawa mikono mara kwa mara, na kuripoti visa vyovyote vinavyohisiwa kuwa na maambukizi kwa kituo cha afya kilicho karibu au kwa kupiga simu namba 199 bure bila malipo.
Serikali, kupitia Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais TAMISEMI, inaendelea na jitihada za ufuatiliaji na udhibiti wa ugonjwa huo, huku wananchi wakihimizwa kuchukua tahadhari ili kujikinga na maambukizi.


Comments
Post a Comment