Na Shomari Binda-Musoma
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan ametuma salamu za pole kwa wananchi wa manispaa ya Musoma waliothiriwa makazi yao kutokana na mvua kali iliyoambatana na upepo iliyonyesha usiku wa kuamkia jana machi 24,2025.
Salamu hizo za pole zimewasilishwa leo machi 25,2025 na mkuu wa mkoa wa Mara Kanali Evans Mtambi alipowatembelea waathirika hao.
Akizungumza kwenye maeneo walikoifadhiwa wananchi hao amesema ametumwa na Rais kufikisha salamu hizo wakati serikali ikiendelea kufanya tathimini kutokana na athari iliyotokea.
Amesema kaya 319 zinadaiwa kuathirika kutokana na taarifa ya awali na msaada wa kibinadamu umeshawafikia walengwa kwenye makambi waliyopo.
Kanali Mtambi amesema katika kipindi hiki upendo zaidi unahitajika kwa wahanga wakati jitihada nyingine zikiendelea.
" Mheshimiwa Rais amenituma niwafikishie salamu za pole katika kipindi hiki kigumu mlichonacho kutokana na athari ya mvua.
" Nitumie fursa hii pia kuwaomba kuzidisha upendo katika kipindi hiki kwenye maeneo ya makambi tuliyopo wakati tathimini na utaratibu mwingine ukiendelea",amesema.
Mkuu huyo wa mkoa amesema licha ya mvua hiyo kuathiri makazi ya wananchi lakini taasisi za umma na mìundombinu ikiwemo ya Tanesco,TTCL,shule na ofisi binafsi zimeathiriwa.
Kwa upande wao wananchi waliofikwa na janga hilo la mvua wamemshukuru Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuwafikishia salamu za pole kupitia mkuu wa mkoa.
Wamesema athari waliyopata ni kubwa na kuiomba serikali kuwaangalia kwa jicho la huruma kuweza kuwasaidia katika kipindi hiki kigumu kwao.





.jpg)
