Chama cha Siasa kinachotawala nchini Uganda National Resistance Movement – NRM kinaripotiwa kutoridhika na matokeo ya uchaguzi mdogo wa ubunge katika eneo la Kawempe Kaskazini.
Inaripotiwa kwamba kamati kuu ya chama hicho iliandaa mkutano kujadili uchaguzi huo mdogo na matokeo yake.
Wajumbe wa kamati hiyo wanaripotiwa pia kujadili kuhusu matukio ya uchaguzi huo kama vile madai ya udanganyifu na vurugu.
Chama hicho kinachoongozwa na Rais Yoweri Museveni hakikuridhika na matokeo ya uchaguzi huo mdogo ambapo Erias Luyimbazi Nalukoola wa chama cha upinzani cha NUP cha kwake Robert Kyagulanyi Maarufu Boby Wine aliibuka mshindi.
Msimamizi mkuu wa uchaguzi katika eneo bunge la Kawempe Kaskazini Henru Makabayi alimtangaza Nalukoola mshindi baada ya kujipatia kura elfu 17, 764.
Chama cha NRM kimetangaza nia ya kuelekea mahakamani kupinga matokeo hayo ambapo mwaniaji wake kwa jina Farida Nambi alijipatia kura 8,593.
Katibu mkuu wa NRM Richard Todwong, alisoma taarifa ya baada ya mkutano wa kamati kuu ya chama.
Aidha Mwenyekiti wa Chama hicho Rais Yoweri Museveni kupitia Taarifa yake aliyoiweka kwenye Mitandao wa X amepinga matokeo ya Uchaguzi kwa madai ya kuwepo kwa Udanganyifu na kukielekeza Chama chake kuwasilisha kesi Mahakamani kupinga matokeo hayo.
Uchaguzi mdogo uliandaliwa katika eneo la Kawempe Kaskazini jijini Kampala kutafuta mbunge mpya kuchukua mahala pa Muhammad Ssegirinya wa chama cha NUP aliyeaga dunia mwezi Januari baada ya kuugua kwa muda mrefu.










Comments
Post a Comment