📍 Ni mradi utakaowanufaisha wakazi wa Kijiji cha Kwatango
📍 Asema ni kazi nzuri za Rais Dkt Samia Suluhu Hassan
📍 Amtaja Waziri Jumaa Awesso kwa kutekeleza miradi mingi Muheza
📍 Awataka wananchi waoneshe shukrani zao kwa kuwaunga mkono
NAIBU Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Hamisi Mwinjuma maarufu MwanaFA, amezindua mradi wa maji katika Kijiji cha Kwatango wenye thamani ya shilingi milioni 679.
Akizindua mradi huo kwenye uwanja wa Kijiji cha Kwatango kilichopo kata ya Kwemingoji wilayani Muheza, MwanaFA alisema mradi huo ni matunda yaliyofanywa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan katika miradi mingi ya maji nchini ikiwemo wilaya ya Muheza.
Alisema mradi huo ni kati ya miradi 17 iliyopo wilayani Muheza ambayo inashughulikiwa na Wakala wa Maji Vijijini (RUWASA) na inagharimu kiasi cha shilingi bilioni 8.4. fedha zote zilizotolewa kwa ajili ya miradi ya maji wilayani Muheza ni shilingi bilioni 11.890.
Alisema wanamshukuru Rais Dkt Samia Suluhu Hassan wakati wa ziara yake mkoani Tanga alizindua mradi wa Maji wa miji 28 katika mkoa wa Tanga ambao utaweza kugharimu kiasi cha zaidi ya shilingi bilioni 100 na kati ya fedha hizo Muheza imetengewa shilingi bilioni 40.
Alisema kabla ya mwaka 2020 wilaya ya Muheza ilikuwa ikipata maji kwa wastani wa asilimia 41 na Sasa katika miaka minne hii wananchi wa Muheza wanapata maji kwa wastani wa asilimia 71.
"Mradi wetu wa Maji wa miji 28 katika wilaya yetu ya Muheza ukikamilika tutakuwa tunapata maji kwa wastani wa juu ya asilimia 95 na utahudumia wananchi wapatao 400,000 katika kata 17 zilizopo wilayani hapa," alisema.
Alisema serikali ya awamu ya sita imekuja kumtua mama ndoo kichwani kutokana na kwamba hapo awali ndoa nyingi zilikuwa zikivunjika kutokana na tatizo la uhaba wa Maji lakini Sasa wananchi wanapata maji karibu.
Alimshukuru Waziri wa Maji na mbunge wa Jimbo la Pangani Jumaa Awesso kwa kumrasishia upatikanaji wa maji katika wilaya hiyo kwakuwa Kila akipita alikuwa akiwaona wananchi wakitaabika na adha ya maji lakini pia mara nyingi alikuwa akimuomba amsaidie shida hiyo.
MwanaFA alisema kuwa kipindi hiki ni cha uchaguzi hivyo akawaomba wananchi wawaunge mkono Rais, Mbunge na madiwani kwa kuwachagua tena ili waendelee kutatua matatizo yao kama ambavyo katika kipindi cha miaka minne hii na ushee wamefanya katika wilaya hiyo tofauti na wakati mwingine wowote.
Awali kaimu Meneja wa RUWASA Omary Kisaka alisema mradi huo ulioanza mwaka jana umetokana na chanzo cha maji cha mto Sigi na kwamba wamejenga vilula 15 katika Kijiji hicho cha Kwatango na utawanufaisha wakazi wapatao 1,500.
Mwakilishi wa Mkuu wa wilaya ambaye ni Ofisa Tarafa ya Muheza Ali Kijazi aliwataka wananchi wautunze mradi huo ili uwe endelevu katika kipindi chote watakachokuwa wakitumia maji hayo.
Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Muheza Erasto Mhina alimshukuru mbunge kwa mradi huo na miradi mingine wilayani humo.
"Mheshimiwa mbunge wetu kwa niaba ya halmashauri tunakuomba utufikishie salamu zetu kwa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwasababu mradi huu umeweza kumtua mama ndoo kichwani na Sasa maji watayabeba mkononi kuyapeleka majumbani," alisema Mwenyekiti huyo.
Diwani wa kata ya Kwemingoji Jerome Jaha alimshukuru mbunge kutokana na kazi kubwa anaifanya ya kuhakikisha anatatua changamoto zilizopo katika wilaya hiyo ikiwemo masuala ya maji, afya, elimu, Miundombinu na huduma za jamii.











Comments
Post a Comment