Mbunge wa Jimbo la Itilima Mkoa wa Simiyu, Njalu Silanga, amemweleza Makamu mwenyekiti wa CCM Tanzania Steven Wasira kuwa Wilaya ya Itilima imeimarisha zaidi huduma za kijamii kwa wananchi, kutokana na Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kutoa fedha nyingi za maendeleo kwa kila sekta.
Mh Njalu ameyasema hayo alipohutubia mkutano wa hadhara katika Kijiji cha Nkoma wilayani humo, katika mapokezi ya Makamu M/kiti CCM Bara, Stephen Wassira.
"Itilima tumejenga kilomita 700 za barabara na tubusasamle (na zaidi) baada ya kuletewa fedha na Serikali ya Awamu ya Tano na ya Awamu ya Sita ya Mama Samia. Tunaishukuru sana Serikali kwa kuwajali wananchi wa Itilima,tumejenga shule za sekondari 12 katika jimbo letu," amesema Mbunge Njalu.
"Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan imetuletea fedha kwa ajili ya kujenga kituo cha kupoza umeme Mkoa wa Simiyu. Zamani tulikuwa na upungufu wa shule, lakini kwa sasa tumejenga shule za madirisha ya vioo. Tunajengewa pia mradi wa maji ya Ziwa Victoria," amesema Njalu,
Njalu huku akishangiliwa na mamia ya wananchi katika mkutano huo,amemweleza makamu mwenyekiti kuwa jimbo hilo pamoja na changamoto ya maji lakini jimbo limepata mabadiliko makubwa ya kimaendeleo katika zote muhimu za kijamii iliwemo ya sekta ya elimu,afya na barabara.
Kwa upande wake Makamu mwenyekiti wa CCM Tanzania bara Steven Wasira amesema sera mpya inakuja kupitia ilani ya uchaguzi ya mwaka 2025-2030 itakaitaka serikali kupeleka matrekta ya kilimo kwenye maeneo yote yenye ukame nchini.
Amesema hatua hiyo inalenga kusaidia wananchi kulima kisasa na kuimarisha uchumi wao.







