Na Shomari Binda-Musoma
MBUNGE wa Jimbo la Musoma mjini Vedastus Mathayo amekamilisha ziara yake ya kutembelea Kata kwa Kata kwa kutangaza kugombea tena nafasi hiyo kwenye uchaguzi mkuu wa 2025 muda utakapofika.
Nia yake ya kugombea tena nafasi hiyo ameitoa leo machi 5/2025 kwenye Mkutano Mkuu wa Kata ya Mshikamano uliohudhuriwa na wajumbe na viongozi wa Chama cha Mapinduzi ( CCM) wa Kata hiyo.
Amesema kutokana na Kata 16 alizofanya ziara kuombwa kugombea tena nafasi hiyo hivyo hana budi kugombea muda utakapofika.
Akielezea utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya mwaka 2020 hadi 2025 amesema utekelezaji umefanyika kwa asilimia kubwa hivyo kila mwana CCM anapaswa kutembea kifua mbele.
Amesema kuanzia sekta ya elimu,maji,afya na miundombinu kwenye Kata ya Mshikamano imetekelezwa na kuwataka wanachama na viongozi kuisemea vizuri serikali ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kila wanapopita.
Mbunge huyo amesema bado ana nguvu na ari ya kuwatumikia wananchi wa jimbo la Musoma mjini na kwenye uchaguzi ujao atagombea tena nafasi hiyo.
" Nawashukuru sana wana Mshikamano kwa kujitokeza kwa wingi kuja kusikiliza kile ambacho tumekitekeleza na nyie wenyewe mmejionea utekelezaji.
" Leo hapa ni Kata yangu ya 16 kutembelea na ndio ya mwisho na kila nilipopita sauti zimesikika zikinitaka kugombea nami kwa kuwa bado nna nguvu za kuwatumikia natangaza kugombea tena muda ukifika",amesema.
Diwani wa Kata ya Mshikamano Njofu Costantine amesema baada ya kuchaguliwa kwenye nafasi hiyo mwaka jana kwenye uchaguzi mdogo kufuatia kifo cha diwani aliyekuwepo mengi yamefanyika kwa muda mfupi akipewa ushirikiano mzuri na mbunge na madiwani.
Amesema kwenye zahanati huduma zimeboreshwa kwa kuongeza vifaa tiba na upatikanaji wa dawa huku sekta ya elimu msingi na sekondari madarasa mapya yamejengwa na mbunge anatengezea madawati,viti na meza kwaajili ya wanafunzi na walimu kukalia.
Kwa upande wao wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Kata ya Mshikamano wameahidi kwenda na mbunge na diwani kwenye uchaguzi mkuu wa 2025.






Comments
Post a Comment