Kampeni ya Ujenzi wa Maabara za Masomo ya Sayansi na Uanzishwaji wa "High Schools" yaendelea Musoma Vijijini
Na Shomari Binda-Musoma
KAMPENI kabambe ya ujenzi wa maabara za masomo ya sayansi na uanzishwaji wa shule za "High Schools" imepamba moto katika jimbo la Musoma vijijini.
Lengo la kampeni hiyo ni kuhakikisha kila shule ya sekondari inakuwa na maabara tatu za masomo ya sayansi ambayo ni Fizikia, Kemia na Bailojia
Akizungumza leo machi 17 2025 na GMTV mbunge wa jimbo la Musoma vijijini Profesa Sospeter Muhongo amesema jimbo linao mradi kabambe wa ujenzi wa maabara hizo tatu kwa kila sekondari ya Kata.
Amesema wanavijiji na viongozi wao wanashirikiana na Halmashauri ya (Musoma DC) na serikali kuu kuchangia ujenzi wa maabara za masomo ya sayansi kwenye sekondari hizo za Kata.
Mbungo Muhongo amesema mradi huo ni kuboresha ufundishaji, ujifunzaji, uelewa na ufaulu wa masomo ya sayansi kwa wanafunzi wa jimboni humo
Amesema uanzishwaji wa "High Schools" za masomo ya sayansi ni muhimu kwani kwa sasa "High School"ipo moja tu nayo ni ya masomo ya "arts"-ambayo ni Kasoma High School.
Muhongo amesema Wizara imetoa kibali cha kufunguliwa "High Schools" mpya mbili za masomo ya sayansi ambazo ni Suguti na Mugango High Schools
Amesema sekondari zenye maabara tatu za masomo ya sayansi zipo 6 na zenye maabara mbili zipo 8 na sekondari zenye maabara moja ni 4 huku sekondari zisizo na maabara ni 8 zikiwa za serikali na sekondari za madhehebu ya Dini za Nyegina maabara 2 na Bwasi 2.
Mbunge huyo amesema bado wanaendelea na kipaumbele cha elimu kutokana na umuhimu wake na kuzitaja sekondari zisizokuwa na maabara kuwa ni Bukwaya (Kata ya Nyegina),Busambara Kata ya Busambara, Ifulifu Kata ya Ifulifu,Murangi Kata ya Murangi,Mtiro Kata ya Bukumi,Nyanja Kata ya Bwasi,Seka Kata yaNyamrandirira na Tegeruka Kata ya Tegeruka
"Tunaombwa tuchangie ujenzi wa maabara tatu za masomo ya sayansi kwenye sekondari hizo nane ambazo hazina maabara.
"Sekondari zenye maabara moja zipo 4 ambazo ni Bukima Kata ya Bukima,Dan Mapigano Memorial Sec Bugoji,Mabuimerafuru Musanja na Kasoma iliyopo Kata ya Nyamrandirira"amesema.
Amesema Mtiro sekondari inakaribia kukamilisha vigezo vya kuanzishwa kwa "High School" ya masomo ya sayansi kwa kuwa maji ya bomba yapo,umeme,bweni la wanafunzi na maabara: zinajengwa
Ameongeza kuwa katika soko la dunia kwenye ajira wana sayansi wanahitajika hivyo upo umuhimu mkubwa wa kuzalisha wana sayansi wengi ili kuendana na soko hilo.



Comments
Post a Comment