Na Dawati la Habari Polisi ;Mwanza
Katika hali isiyo ya kawaida, mkazi wa Kijiji cha Mwanekeyi, Wilaya ya Kwimba, mkoani Mwanza, Shaban Lyahasi (24), ameangua kilio mahakamani alipotakiwa kujitetea kabla ya kusomewa hukumu katika kesi ya ubakaji iliyokuwa inamkabili.
Lyahasi amesomewa hukumu hiyo katika Mahakama ya Wilaya ya Kwimba mkoani Mwanza na kupewa adhabu ya kifungo cha miaka 30 jela baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la kumbaka mwanafunzi wa darasa la saba, (15), (jina linahifadhiwa kwa sababu za kisheria).
Hukumu hiyo katika kesi namba 26610/2024 imesomwa leo Machi 12,2025 na Hakimu mkazi mwandamizi, John Chai Jagadi wa mahakama hiyo mbele ya Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Juma Kiparo.
Imedaiwa mahakamani hapo kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo tarehe 05. 09. 2024 huko katika Kijiji cha Mwamanga Wilayani humo ndani ya chumba chake huku akimuahidi binti huyo kuwa atamuoa kinyume na kifungu 130 (1)(2)(e) na 131(1) vya kanuni ya Adhabu, sura ya 16 ya sheria marejeo ya mwaka 2022.
Mshtakiwa alifikishwa Mahakamani tarehe 18.09.2024 na kusomewa shtaka lenye kosa la kubaka na mwendesha mashtaka ambapo alikana kutenda kosa hilo jambo lililopelekea mwendesha mashtaka kwa niaba ya Jamhuri kuita mashahidi wanne akiwemo mwathiriwa wa kitendo hicho.
Baada ya Hakimu, Jagadi kusikiliza mashahidi wote wanne wa jamhuri aliona kwamba mshtakiwa alikuwa na kesi ya kujibu na hivyo kumtaka aweze kujitetea.
Baada ya kupewa nafasi hiyo mshatakiwa alishindwa kujitetea na kuangua kilio mbele ya mahakama hiyo.
Aidha, mwendesha mashtaka aliomba Mahakama kutoa adhabu kali kwa mtuhumiwa kwa kuwa vitendo hivyo vya ukatili kwa wanawake vimekuwa vingi ambavyo vinasababisha mabinti kushindwa kumaliza shule na hivyo kufifisha juhudi za serikali za kuwawezesha watoto wa kike kushindwa kufanikiwa.
Hata hivyo kilio hicho hakikuweza kuzaa matunda kwa kumuondoa katika shtaka hilo na hivyo Hakimu Jagadi kumhukumu kutumikia jela miaka 30 pamoja na kulipa fidia ya shilingi laki tatu kwa binti aliyetendewa ukatili huo.



Comments
Post a Comment