Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene ameipongeza timu inayosimamia mchakato wa ajira za Ualimu, kwa namna wanavyoendesha zoezi hilo kwa uadilifu na ufanisi.
Simbachawene ametoa pongezi hizo leo Februari 23, 2025, alipotembelea na kukagua timu inayosimamia mchakato wa ajira za Ualimu inayoendelea na kazi hiyo katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) mkoani Morogoro.
Ametumia fursa hiyo kuwaita ofisini kwake Dodoma kwa mazungumzo viongozi wa vijana waliojitambulisha kwenye andiko lao kuwa ni 'Non Employed Teachers Organisation (NETO)' wenye umoja wao kupitia mitandao ya Kijamii.
“Nimesoma makala yao yenye kichwa cha habari Ombi la Wahitimu wa Ualimu Vyuo mbalimbali nchini kati ya mwaka 2015-2023 kwa Serikali, andiko lao ni zuri na linaeleweka ingawa linahitaji ufafanuzi zaidi, hivyo ninatoa wito kwa vijana hao kuja ofisini Dodoma kwa mazungumzo”. amasisitiza Waziri Simbachawene
Amesema amewasiliana na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Adolf Mkenda na viongozi wa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), na wamekubalina kushiriki mazungumzo hayo wakati kundi hilo litakapokuwa tayari.

Comments
Post a Comment