MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Chama Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Stephen Wassira, ameiagiza Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, kuhakikisha ardhi ya vijiji iliyoporwa kinyume cha sheria, inarudishwa kwa wananchi.
Wasira alitoa maagizo hayo leo jijini Dodoma, wakati akizungumza na viongozi pamoja na wanaCCM waliojitokeza kumpokea katika Ofisi za Makao Makuu ya CCM.
Alisema kuna watu wamejimilikisha ardhi kwa kutoa rushwa jambo ambalo CCM inaakataa kwa nguvu zake zote.
“Haki ya Watanzania kumiliki ardhi ni sera ya msingi kwa CCM. kuna watu wanajimilikisha maeneo makubwa na hawayaendelezi kwa kutoa rushwa. Tunaomba maeneo yote ambayo yanamilikiwa kinyume cha sheria yarudishwe kwa wananchi,” alisisitiza.
“Tunataka kuona watu wakipata matatizo sehemu yao sahihi ambayo wanaweza kupata ufumbuzi iwe CCM. Hivyo tunaendelea kuhamasisha kuwa kitu kimoja. Hii ni muhimu hasa kipindi hiki tunapoelekea katika uchaguzi mkuu, lazima tuungane ili tushinde kwa kishindo.
"Nasisitiza CCM tuache migogoro bali tufanye kazi ya kutatua shida za watu,hiki chama ni chama cha wanyonge hivyo lazima tufanye kazi ya kutatua matatizo ya wananchi kuanzia ngazi za matawi"alisema
Hata hivyo alisema milango ipo wazi CCM kwa yoyote mwenye shida na anayehitaji mazungumzo lakini ccm haiwezi kukubali mazungumzo yenye masharti.
Mzee Wassira amesema katika uchaguzi mkuu unaotarajia kufanyika badae mwaka huu ccm lazima ishinde na ishike dola na kwamba kama chama kikubwa cha siasa barani Afrika hilo halina mjadala na kwamba vyama vingine vidogo vitaendelea kuchezea ndevu za babu zao wakati ccm (babu)ikiendelea kuongoza dola katika kulinda amani ya nchi.
"Kuna watu wanasema eti CCM imeongaza muda mrefu,nawashangaa sana hawa wanahoji jambo hili,watuambie wakati tunadai uhuru tuliwambia tutaongoza muda gani?wao ni wajukuu si kosa kuchezea ndevu za babu na wataendelea kuchezea maana ndio kazi wanayoijua"alisema Wassira na kushangikiwa.
CCM mkoa wa Dodoma ulifanya mapokezi makubwa ya makamu huyo wa CCM mwenyekiti Tanzania bara yaliyopambwa na maandamano wakiwemo vijana wa CCM na bodaboda.