Serikali Mkoani Mara yamshukuru Rais Dkt. Samia Ujio wa Madaktari Bingwa na Bobezi Kuhudumia Wananchi
Na Shomari Binda-Musoma
SERIKALI mkoani Mara imemshukuru Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa ujio wa madaktari bingwa na bobezi na kuweza kuwahudumia wananchi.
Shukrani hizo zimetolewa na Katibu Tawala wa mkoa wa Mara Gerald Kusaya kwa niaba ya mkuu wa mkoa wa Mara Kanali Evans Mtambi wakati wa kufunga kambi ya siku 5 ya madaktari hao.
Akizungumza kwenye hafla ya shukrani kwa madaktari waliokuwa wameweka kambi kwenye hospital ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Kusaya amesema wananchi 2,244 wamefanikiwa kuonwa na kutibiwa.
Amesema kati ya hao 74 wamefanyiwa upasuaji na 46 wamepewa rufaa ya kwenda hospital ya rufaa ya kanda Bugando kwa matibabu zaidi.
Katibu Tawala huyo amesema kambi hiyo imefanikiwa kukusanya shilingi milioni 186 na kutoa shukrani kwa madaktari hao kutokana na kazi kubwa waliyoifanya.
" Tunawashukuru sana madaktari kwa kazi kubwa na nzuri mliyoifanya kwa kuja na kufanikiwa kuwatibu wananchi hapa Mara.
"Tunamshukuru pia Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutuletea madaktari bingwa na bobezi hii ikiwa no mara ya pili", amesema.
Kwa upande wao wananchi waliofikiwa na madaktari hao wametoa shukrani na kuomba huduma hiyo kuwa endelevu kwa kuwa ni msaada kwao.
Wamesema wanapokuja madaktari hao gharama za kuwafuata kwenye hospital za nje zinapungua na kupata huduma karibu.

Comments
Post a Comment