Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Jumanne Sagini amekutana na kufanya mazungumzo na Naibu Katibu Msaidizi Ofisi ya Kimataifa ya Madawa ya Kulevya na Masuala ya Utekelezaji wa Sheria Maggie
Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Jumanne Sagini amekutana na kufanya mazungumzo na Naibu Katibu Msaidizi Ofisi ya Kimataifa ya Madawa ya Kulevya na Masuala ya Utekelezaji wa Sheria Maggie Nardi kwa ajili ya kuangalia namna bora ya kuimarisha ushirikiano katika masuala ya Usaidizi wa Kisheria na uhalifu ili kusaidia katika kupambana na uhalifu wa kupangwa wa kimataifa katika kanda.
Akizungumza katika kikao hicho kilichofanyika Jijini Dar es salaam Disemba 06,2024 Mhe Sagini amesema kuwa Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali ili kudhibiti wimbi la usafirishaji haramu wa Binadamu ikiwemo kutunga sheria ya kuzuia usafirishaji haramu wa binadamu, Kuanzishwa kwa Kikosi Kazi cha Ulinzi wa Watoto wa Usafirishaji Haramu wa Binadamu mwaka 2022 na hatua nyingi zaidi ikiwemo kuzinduliwa kwa Mwongozo wa Ulinzi na Utunzaji wa Mashahidi mnamo Mei 2023.
Sagini ameongeza kuwa mbali ya kuwepo kwa muendelezo wa mafunzo kwa waendesha mashtaka na wapelelezi bado nguvu kubwa inahitajika zaidi ili kuongeza idadi ya wataalamu watakaopatiwa mafunzo ya usimamizi wa sheria kuhusu masuala yanayohusiana na usafirishaji haramu wa binadamu ili kudhibiti kabisa usafirishaji haramu wa Binadamu.
Aidha Sagini ameahidi kuwa serikali ya Tanzania itaendelea kuimarisha urafiki,ushirikiano na mahusiano mazuri yaliyopo baina yake na Marekani.
Kwa upande wake,Naibu Katibu Msaidizi Ofisi ya Kimataifa ya Madawa ya Kulevya na Masuala ya Utekelezaji wa Sheria Mhe.Maggie Nardi ameipongeza Serikali ya Tanzania kwa kuweka sheria na mifumo mbalimbali mathubuti katika kupambana na biashara haramu na kusema kuwa ofisi yake ipo tayari kushirikiana kwa namna yoyote kuendelea ili kuboresha mbinu na ufanisi katika kuthibiti biashara hizo











Comments
Post a Comment