Jinsi Mashine za Kusaga za Solar Zilivyo Suluhisho Mbadala wa Mashine za Mafuta Katika Gharama za Uendeshaji na Uhifadhi wa Mazingira
Na Emmanuel Chibasa
Mashine za kusaga ni vifaa vinavyotumika kusaga na kukoboa nafaka Kwa ajili ya kupata chakula kutoka Katika mazao mbalimbali kama vile mahindi, mihogo, ulezi, mtama, mpunga pamoja na bidhaa nyingine za kilimo.
Kuna aina tofauti za mashine za kusaga nafaka ambazo pia zinatumia vyanzo tofauti vya uzalishaji wa umeme, ambazo ni mashine zinazotumia umeme wa gridi, mashine zinazotumia mafuta ya dizel pamoja na mashine zinazotumia nishati ya umeme jua yani Solar.
Katika maeneo ya vijijini bado kuna baadhi ya maeneo ambayo hayajafikiwa na umeme wa gridi, wananchi wanatumia mashine za kusaga zinazotumia mafuta zinaendeshwa kwa kutumia injini inayotumia mafuta ya diseli kama chanzo cha nguvu kuendesha mfumo wa magurudumu na gia zinazowezesha nafaka kukobolewa na kusagwa.
Katika makala yetu leo, George Marato Tv Tunaangazia huduma za kusaga nafaka kwa mashine zinazotumia mafuta ya disel kwa kuangalia changamoto za gharama za uendeshaji na uhifadhi wa mazingira lakini pia kuangalia matumizi ya teknolojia ya nishati ya jua yani Solar, inavyoweza kusaidia kutumika kama mbadala wa matumizi ya mashine za mafuta Katika maeneo ambayo hayajafikiwa na umeme wa gridi kama suluhisho la Kupunguza gharama za uendeshaji wa biashara hiyo pamoja uhifadhi wa Mazingira Kwa wananchi wa wilaya ya Musoma Mkoani mara.
Kisiwa cha Rukuba ni miongoni mwa visiwa vinavyopatikana Ziwa Victoria katika Wilaya ya Musoma mkoa wa Mara, ambapo kutokana na eneo la ardhi sehemu kubwa kuzungukwa na maji, bado kisiwa hiki hakijafikiwa na huduma ya umeme wa gridi, hali inayopelekea wakazi wa eneo hilo, kutegemea nishati ya umeme jua pamoja na jenereta zinazotumia mafuta kupata huduma ya umeme kupata mwanga pamoja na Kuendesha shughuli mbalimbali za ujasiliamali zinazotegemea nishati ya umeme Ikiwa ni pamoja na matumizi ya mashine za kusaga nafaka zinazotumia mafuta ya disel ambazo zinatajwa kuwa na changamoto za gharama za uendeshaji na uchafuzi wa mazingira.
Licha ya mashine za kusaga zinazotumia mafuta ya disel kutajwa kuwa na changamoto ya gharama katika uendeshaji pamoja na wataalam wa maswala ya Mazingira kueleza kuwa zinachafua pia mazingira kutokana na moshi wa mafuta wakati wa kusaga, lakini baadhi ya watumiaji wa mashine hizo wanasema pia kuna faida zake ikiwa ni pamoja na kupatikana kwa urahisi hususani katika maeneo yasiyo na umeme wa gridi kama vile maeneo ya visiwa.
Mbali na faida hizi lakini watumiaji wa mashine hizi pia wanasema zipo changamoto kadhaa zinazowakabili kama vile, gharama kubwa za uendeshaji kwa bei ya mafuta ya disel kuzidi kuongezeka hasa maeneo ya vijijini, ambapo hakuna vituo vya kuuza mafuta kama ilivyo maeneo ya mjini, gharama za matengenezo ambapo Injini zinahitaji kubadilisha mafuta, vipuri, na mara nyingine kuitaji matengenezo makubwa lakini hakuna maduka yanayouza Vifaa Katika maeneo Yao.
Jumanne Milunda, mkazi wa kisiwa cha Rukuba, anayejishughulisha na biashara ya mashine ya kusaga inayotumia mafuta ya disel kwa miaka muda sasa, anasema kutokana na kukosekana kwa umeme wa gridi katika kisiwa hicho wakazi wa eneo hilo utegemea mashine hiyo ya kusaga inayotumia disel kusaga nafaka kwa ajili ya chakula.
“Nimewekeza kwenye biashara hii ya mashine ya kusaga inayotumia mafuta kutoka na huku hakuna Huduma ya umeme wa Tanesco au ule wa REA, lakini changamoto ni kubwa. Mafuta ni ghali sana, tunalazimika kuyasafirisha kutoka mji wa Musoma kwa boti hiyo pia ni gharama tutatumia Katika Biashara hii Kila siku na inamaana mafuta yakikosa basi huduma nayo inasimama.
Muda mwingine mashine inaharibika na huku tulipo hakuna duka la vifaa hivyo inakubidi uagize huko mjini, jambo linalolazimu kusimamisha biashara kwa siku kadhaa na Kwa kweli, kama Teknolojia hiyo ipo basi watuletee sababu itakua mbadala wa kutusaidia Katika gharama za uendeshaji na wakazi watapata Huduma Kwa bei nafuu na rahisi zaidi.” Amesema Milunda
Naye Bwire Mkama mfanyabiashara ya mashine Musoma anasema awali alikua anatumia mashine ya kusaga inayotumia mafuta ya disel na kero aliyokua anaipata ni namna ya kuiwasha mashine hiyo Pindi anapopata wateja.
"Kero kubwa niliyokua naipata ni wakati wa kuwasha mashine unatumia nguvu kubwa kuzungusha Kwa mkono handle mpaka mashine ikubali kuwaka unakua umetumia nguvu sana, Sasa Ile kuwasha mara Kwa mara inachosha sababu sio kama zile za umeme unabonyeza tu swichi mashine inawaka na unabonyeza sehemu ya kuzima inazima
Pia mashine hizo uwezi kusaga nafaka kigodo kama ilivyo hizi zinatumia umeme mtu anaweza kuja na hata kilo mbili ukamsagia lakini Ile ya mafuta ukisaga kama hivi unajikuta unapata hasara kwenye mafuta, zile zinahitaji upate wateja wengi ufanye Kazi Kwa mara moja ndio utaiona faida"Amesema Bwire
Kwa upande chausiku Mgeta mama wa familia na mkazi wa kisiwa hicho anasema hawana njia nyingine mbadala ambayo inawawezesha kusaga nafaka zao ili kupata unga kama ilivyo maeneo ya mjini ukinunua mahindi au udaga kwenye mshine haulipi tena hela ya kusaga kwa sababu mashine ni nyingi na zinatumia umeme lakini huku kwetu kutokana na mashine kuwa chache na zinatumia mafuta kwa debe moja tunasaga kwa kuanzia Shilingi 1000 hadi 1500.
Changamoto hii inayompata Jumanne Milunda na aliyopitia Bwire Mkama pia inawapata watoa huduma wengine katika maeneo ya vijijini katika maeneo ambayo hayajafikiwa na umeme wa gridi, lakini wakipatiwa elimu ya matumizi ya teknolojia ya mashine za kusaga zinazotumia nishati ya umeme jua itakua suhulisho Katika kuondokana na Changamoto hizo katika kutoa huduma Kwa Wananchi.
Mashine za kusaga zinazotumia nishati ya jua zinatajwa kuchukua nafasi kama suluhisho endelevu katika kupunguza gharama za uendeshaji na rafiki kwa mazingira sababu zinatumia paneli za jua kukusanya nishati, ambayo inahifadhiwa kwenye betri au kutumika moja kwa moja kuendesha mashine bila Kutoa moshi unaochafua hewa
Faida kubwa zinazotajwa na wataalam wa nishati ya umeme jua katika matumizi ya mashine ya kusaga inayotumia solar, ni pamoja na kutumia gharama nafuu za uendeshaji ambapo mtumiaji atakua hana haja ya kununua mafuta mara kwa mara ili kutoa huduma hiyo kwa wateja wake, mashine hizo hazitoi moshi wala kelele, ni rafiki kwa maeneo ya mbali ambayo hayahitaji miundombinu ya umeme wa gridi, hivyo yanafaa vijijini lakini pia nishati ya jua ni ya bure na inapatikana kwa urahisi.
Innocent Mwita ni mtaalam wa nishati mbadala anasema kuna faida kubwa kwa watoa huduma wa mashine za kusaga nafaka na bidhaa nyingine za kilimo katika kuwekeza hasa katika maeneo ya vijijini ambayo hayajafikiwa pia na umeme wa gridi
"Mashine hizi zinatoa fursa kwa wajasiriamali wa vijijini kuwekeza katika biashara ya kusaga nafaka kwa gharama ndogo, wafanyabiashara wa vijijini wakiwekeza katika teknolojia hii wataona jinsi teknolojia hii ilivyo suluhisho katika kuwasaidia l kupunguza gharama za uendeshaji na kuongeza faida.
Pia anatoa wito kwa serikali kuweka mazingira wezeshi kwa uwekezaji wa nishati ya jua kwa kuendelea kutoa ruzuku kwa mashine hizi, kuweka sera bora za nishati mbadala, na kutoa elimu kwa wananchi. Ikiwa tutafanya hivi, tunaweza kusaidia vijiji kama Rukuba kupunguza umasikini na kuboresha maisha ya watu." Amesema Mwita.
Mkurugenzi wa teknolojia ya nishati jadidifu wa wakala wa nishati vijijini(REA) Mhandisi Advera Mwijage akiwa mkoani Kagera tarehe 7 Novemba 2024, alisema kuwa serikali imetenga shilingi bilioni 8 kupitia kwa wakala wa nishati vijiji(REA) kwa ajili ya kusambaza umeme ndani ya visiwa 118 vilivyopo maeneo mbalimbali nchi nzima.
“Serikali imetenga fedha hizo ili kuwafikishia wananchi wote wanaoishi maeneo ya visiwa na yale ambayo sio rafiki kufikiwa na gridi ya taifa na ilisaini mkataba na benki ya dunia ili kuwezesha upatikanaji wa nishati ambayo ni salama kwa Tanzania.” Alisema Advera
Serikali inatekeleza Mpango Mkuu wa Nishati Vijijini (REMP) 2022/23 hadi 2029/30 ambao unasaidia utekelezaji wa lengo la Tanzania la kupanua upatikanaji wa huduma za nishati za kisasa katika maeneo ya vijijini, sambamba na Lengo namba 7 la Maendeleo Endelevu (SDG 7) na Ajenda ya Utekelezaji wa Serikali ya SE4All (Nishati kwa Wote).
Wakati mashine za kusaga za disel zimekuwa nguzo muhimu kwa jamii za vijijini ambapo umeme wa gridi haujafika, changamoto zake zinafanya matumizi ya mashine za solar kuwa suluhisho bora. Uwekezaji wa serikali, mashirika binafsi, na wajasiriamali katika teknolojia ya nishati ya jua ni hatua muhimu kuelekea maendeleo endelevu na kupunguza umasikini kwa jamii ambazo hazijafikiwa na miundombinu ya umeme wa gridi.




.jpg)









.jpg)
Comments
Post a Comment