Tarafa ya Mbarika yajivunia ongezeko la ufaulu kidato cha nne na darasa la saba

GEORGE MARATO TV
0


Tarafa ya Mbarika wilayani Misungwi Mkoani Mwanza imefanikiwa kutokomeza ufaulu wa Daraja sifuri katika Matokeo ya Mitihani ya Taifa ya kidato cha nne.

Tarafa hiyo pia inajivunia ongezeko la ufaulu wa wahitimu wa elimu ya msingi kutoka asilimia 48 mwaka mwaka Jana hadi kufikia asilimia 72 mwaka huu.


Mafanikio hayo yamefikiwa kufuatia ushirikiano uliopo baina ya wadau mbalimbali wa sekta ya elimu wakiwemo wazazi na walezi,walimu pamoja na viongozi wa ngazi zote pamoja na uwekezaji unaofanywa na serikali kwenye sekta ya elimu.


Afisa Tarafa hiyo Cresensia Mwalongo amebainisha hayo wakati ziara ya kuzungumza na wanafunzi wa shule mbalimbali za sekondari zilizopo kwenye Tarafa hiyo ikiwemo Mbarika,Mnyeti,Ilujamate na Lubili.

‘’Tunazunguka kwa ajili ya kuzungumza na wanafunzi kuwatia moyo na kuwaonyesha hali ya Maisha ambayo iko nje ambapo kama wakifanya vibaya watakwenda kuishi namna gani,kwa hiyo tunawatia moyo na kuwahamasisha kuhakikisha wanajikita zaidi katika masomo na kuachana na mambo yasiyofaa kama wanafunzi’’alisema Mwalongo na kuongeza kuwa

‘’Lakini pia tunazungumza na walimu na kusikiliza changamoto zao,zile ambazo ziko ndani ya uwezo tunazitatua na zilizo nje ya uwezo wa Tarafa hii tunazifikisha mbele ili ziweze kufanyiwa kazi na zaidi ya hapo kama Tarafa katika ziara hii tumetoa zawadi ya kitarafa,walimu wetu tumewapa mifuko ya saruji,sukari na zawadi nyinginezo ikiwa ni motisha ya kuwasaidia walimu na kuwatia moyo na kuwapa nguvu ili waweze kufanya kazi zaidi kwenye program hiyo ya kutokomeza zero’’

Kampeni ya kutokomeza ziro ilianza mwaka 2019 katika Tarafa ya mbarika kufuatia Tarafa hiyo kuwa na ufaulu duni ambapo ushirikiano baina ya wadau mbalimbali wa sekta ya elimu wakiwemo wazazi na walezi,walimu pamoja na viongozi wa ngazi zote pamoja na uwekezaji unaofanywa na serikali kwenye sekta ya elimu ndio uliofanikisha mafanikio hayo.


Afisa Tarafa ya Mbarika Cresensia Mwalongo ameishukuru serikali kuu kwa kutoa shilingi millioni 40 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa bweni la wasichana katika shule ya sekondari Mbarika.

Mwalongo amesema kuwa kukamilika kwa ujenzi wa bweni hilo kutawaondolea watoto wa kike changamoto nyingi ikiwemo adha ya kutembea umbali mrefu pamoja na vishawishi vinavyomkumba mtoto wa kike na hatimaye kuongeza zaidi ufaulu.

‘’Na imani kwamba tukifanikiwa kukamilisha bweni hili,wanafunzi watafaulu zaidi ya hapa,kama tulikuwa hatuna divisheni zero kwa miaka mitano basi tutakuwa na divisheni one na two na walimu wapo kidedea kuhakikisha hilo linafikiwa,kwa hiyo tunaishukuru sana serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutuwezesha kupata madarasa mapya  ya kutosha kwenye kila shule’’alisema Mwalongo

Akizungumza wakati wa ziara hiyo,Mwalongo pia amewataka wanafunzi kujiepusha na mambo yanayoweza kukwamisha kufikia ndoto zao ikiwemo kujihusisha na mapenzi wakiwa shule pamoja na kucheza kamari na badala yake wazingatie masomo kikamilifu ili waweze kupata ufaulu mzuri utakaowawezesha kusonga mbele.


Kwa upande wao,baadhi ya walimu wa shule za sekondari zilizoko Tarafa ya Mbarika wamesema kuwa elimu iliyotolewa na afisa tarafa imewapa ari na nguvu mpya ya kufanya kazi kwa bidii zaidi.



Nao wanafunzi wamesema kuwa elimu iliyotolewa imewajengea uwezo wa namna ya kuepuka vishawishi vinavyoweza kukwamisha kufikia ndoto zao za kitaaluma.








Wanafunzi hao wakiwemo wa shule za sekondari Mbarika,Mnyeti,Lubili na Ilujamate wamesema baada ya shule zao kufuta divisheni ziro,malengo yao sasa ni kufuta ufaulu wa daraja la nne na la tatu kuanzia mwaka huu na miaka ijayo.







 


Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
Post a Comment (0)

#buttons=(Accept !) #days=(20)

Our website uses cookies to enhance your experience. Learn More
Accept !
To Top