Na Zainab Ally, Mikumi.
Taasisi ya Mama Ongea na Mwanao,inayoundwa na wasanii mbalimbali wa kuigiza pamoja na nyimbo za Bongo Fleva imevutiwa na vivutio vinavyopatikana Hifadhi ya Taifa Mikumi mkoani Morogoro ambapo wameahidi kuwa mabalozi wa kutangaza hifadhi hiyo hapa nchini.
Kiongozi wa ziara hii ya watu zaidi ya 20,Steve Mengele alisema jana tarehe 7/11/2024 kwamba wasanii wote waliotembelea hifadhi hiyo wamevutiwa sana na wanyama wanaopatikana Mikumi wakiwemo ‘Big Four’ ambapo alisema kuwa atahakikisha ziara hiyo inatumika kuitangaza Hifadhi ya Taifa Mikumi.
“Tumefurahishwa sana na utalii wetu tulioufanya katika Hifadhi hii ya Taifa Mikumi,tumeweza kuwaona wanyama mbalimbali wakiwemo ‘Big Four’ ambao ni simba,chui,tembo na nyati,hivyo furaha yetu haitaishia hapa kwani sisi kama wasanii tunaahidi kuitangaza hifadhi hii ya Mikumi”alisema Mengele.
Aidha Mengele maarufu kwa jina la Steve Nyerere aliipongeza serikali inayoongozwa na rais Dk Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa miradi mbalimbali inayoendelea kujegwa ndani ya hifadhi hiyo.
Alisema ujenzi wa barabara,kiwanja cha ndege na nyumba za wageni utakapokamilika utafungua fursa kwa watalii wengi zaidi kuja kutalii katika hifadhi hiyo na kwamba wasanii nchini wataendelea kumuunga mkono mama Samia katika harakati zake za kutangaza vivutio vyote vilivyopo nchini.
“Tunaona jinsi serikali yetu ilivyokuza sekta ya utalii hapa nchini,sisi kama wasanii tutaendelea kuunga mkono juhudi hizo,nawaomba watanzania wengine tunapoelekea mwisho wa mwaka,badala ya kwenda Dubai waje hapa Mikumi kutalii”alisema Mengele.
Naye Yusuph Mlela alisema amefarijika sana kufika mara ya kwanza Hifadhi ya Taifa Mikumi kwa ajili ya kufanya utalii wa ndani ambapo alieleza kuwa kutokana na kufurahishwa na mandhari mazuri ikiwa ni pamoja na vivutio vinyavyopatika, watanzania hawana haja kwenda kutalii nchi za nje.
“Raia wa kigeni wanaongoza kuja nchini kutalii na hii ni kwa sababu ya sifa za vivutio vilivyopa nchini hasa Mikumi rai yangu kwa watanzania badala ya kwenda nchi kama Dubai na kwingineko waje hapa Mikumi kwa ajili ya kufanya utalii”alisema Mlela
Kwa upande wake Afisa Mwandamizi wa Wizara ya Maliasili na Utalii,Mariam Mafile aliipongeza Taasisi ya Mama Ongea na Mwanao kwa kitendo cha kufanya utalii katika Hifadhi ya Taifa Mikumi kwani ni moja ya njia ya kuitangaza ambapo aliwataka wasanii hao kuitangaza zaidi hifadhi hiyo na kuwa mabalozi wa kuzitangaza zaidi Hifadi za taifa zilizipo nchini.
Mkuu wa hifadhi hiyo, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi ,Augustine Massesa alisema Hifadhi ya Taifa Mikumi imekuwa ikitanuka kila siku na hii ni kutokana na juhudu za Raisi Dk Samia Suluhu Hassan za kukuza sekta ya utalii nchini.
Aidha assesa aliwashukuru wasanii hao kwa kuitembelea hifadhi hiyo na kwamba Menejimenti ya Mikumi kwa ujumla inauhakika kwamba wasanii hao watakuwa mabalozi wazuri wa kuitangaza Hifadhi ya Taifa Mikumi kitendo ambacho kitazidi kuyavuta makundi mbalimbali ya watu kwenda kutalii.












