Na Ghati Msamba- Mara
Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi, amemuagiza Afisa Madini wa Mkoa huo, Amin Msuya, kusitisha uchaguzi wa viongozi wa mgodi wa Irasanilo, uliopo Buhemba, Wilaya ya Butiama, na kupitia upya kanuni na katiba ya Kikundi cha Wachimbaji Wadogo wa mgodi huo ndani ya siku 21.
Ameyasema hayo kwenye kikao cha Wachimbaji Wadogo na viongozi wao kilichofanyika katika ukumbi wa uwekezaji wa mkoa huo.
Lengo la kikao hicho ni kutatua changamoto za migogoro iliyopo baina ya wachimbaji wadogo na viongozi ili kila mmoja wao apate misingi stahiki ya kiutawala.
Amewataka pia wachimbaji kuachana na tabia za kujiwekea makundi ambayo hayatawasaidia lolote na badala yake wabadilike na waungane kwa pamoja ili waweze kujikuzia uchumi na kuendelea kusimamia shughuli za mgodi, ili viongozi waliokuwepo wapishe uchunguzi.
"Nimefuatilia hiki Kikundi kingetulia mngekuwa mbali, na mngekuwa mmeishaanzisha mradi wa ujenzi wa hoteli kubwa ambayo ingeweza kuwa chanzo cha kuwakuzia uchumi," Amesema Mtambi.
Aidha, mnamo Januari 15, 2024, Mkuu wa Wilaya ya Butiama, Moses Kaegele, alifanya kikao kilichowakutanisha pamoja Afisa Madini mkazi wa Mkoa wa Mara, viongozi wa mpito, na wawakilishi wa wanachama.
Katika kikao hicho, ilielekezwa kuwa viongozi wa muda wahudumu kwa siku 30 kuanzia tarehe ya kikao. Afisa Madini alielekezwa kubainisha majukumu yanayoweza/yasiyoweza kufanywa katika kipindi hicho cha uongozi wa muda.
Majukumu hayo ni kusimamia katiba ya kikundi, kusimamia na kuhakikisha shughuli za mgodi zinaendelea, kusimamia na kuhakikisha mapato ya kikundi na serikali yanakusanywa kwa mujibu wa taratibu zilizopo, kuwasilisha kikundi kwenye shughuli za nje ya kikundi, na kusimamia kulinda mali za kikundi.
Pia, viongozi wa mpito hawakutakiwa kusaini mikataba ya aina yoyote, kutokuajiri au kufukuza waajiriwa wa mgodi kwa kipindi hicho, kutoitisha uchaguzi wa aina yoyote ile, kutovunja au kutengua wajumbe wa kamati tendaji na kamati ya uongozi, na kutekeleza majukumu mengine ambayo hayataathiri taswira na ufanisi wa mgodi kwa ujumla.
Mkuu wa Mkoa amesema kuwa baada ya kusikiliza kero za wachimbaji, amebaini kuwa tatizo la Katiba na uongozi linahitaji hatua za haraka.
"Naagiza kamati yangu ya mgogoro, wanasheria, Afisa Ushirika, Afisa Maendeleo, na Mkuu wa Wilaya ya Butiama, kaeni na wachimbaji, mtakalia hapa Musoma au Butiama, kabla ya Ijumaa mkiangalia kama mtakuwa mmepitia Katiba hiyo na kutoa mapendekezo. Wiki ijayo, mnipatie rasimu hiyo ili niipitie," alisema Mkuu Mtambi.
Afisa Madini wa Mkoa wa Mara amesema kuwa ofisi ya madini ipo tayari kushirikiana na wachimbaji ili kuhakikisha mgodi unaendelea kufanya kazi vizuri na kuwa chanzo cha ajira stahiki.
Afisa Madini amesema walizuiwa baadhi ya majukumu kwa sababu viongozi wa mpito ni wa muda wa mwezi mmoja. Hata hivyo, Mwenyekiti na Katibu wa kikundi wanaendelea na majukumu yao kama viongozi wa muda.
Katibu wa muda wa Kikundi cha Irasanilo, Malima Bunyoga, amesema anatamani uchaguzi ufanyike kwa sababu hata yeye amepewa mipaka ya kazi, jambo ambalo limesababisha ashindwe kuwajibika ipasavyo. Alitoa malalamiko kuhusu Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kutoza gharama za matumizi ya umeme kwa makadirio badala ya malipo kupitia mfumo wa Luku.
"Umeme tunaolipa kwa TANESCO ni kwa makadirio, hatulipi kwa mfumo wa Luku. Kwa kipindi nilichokaa kwenye ukatibu, tangu Januari hadi Oktoba, tumelipa TANESCO zaidi ya Tsh. Milioni 182," amesema Malima.
"Malipo ya bili ya umeme mwaka 2024: Januari, Tsh. 5,484,558; Februari, Tsh. 7,480,932; Machi, Tsh. 19,424,512; Aprili, Tsh. 21,491,753; Mei, Tsh. 21,191,930; Juni, Tsh. 24,302,143; Julai, Tsh. 19,537,318; Agosti, Tsh. 18,674,079; Septemba, Tsh. 16,392,015; Oktoba, Tsh. 14,267,934; na Novemba, Tsh. 14,581,981, jumla ya fedha zote ni Tsh. 182,829,154," amesema Malima.
Ameongeza: "Mimi nimefungwa na majukumu, sihusiki tena kufanya kazi kwasababu mimi ni wa muda. Mgodi sio kwamba hautoi hela, unatoa hela lakini cha ajabu, mgodi hauna hela. Wakati tunaanzisha mgodi, watu tuliuza kuku."
"Uchaguzi unachelewesha mambo, uchunguzi unafanyika kwa gharama kubwa. Walitaka Tsh. Milioni 15 kwa uchunguzi wa awamu ya pili, tukavutana na tukataka watufanyie kwa Tsh. Milioni 4, lakini wilaya ililazimisha zikafika Tsh. Milioni 9. Viongozi wa wilaya wanaomba hela," amesema Malima.
"Wanafagilia wale wapigaji akikupa elfu 20,000 unasema fulani mzuri, huu mgodi ni wa kindugundugu. Halmashauri inatuumiza inatoza ushuru Tsh. 1,000 kwa kila kiroba chenye mawe yanayodhaniwa kuwa na dhahabu. Hiyo pesa ni kubwa sana na haitoi risiti ya mapato. Halmashauri haituletei faida itokanayo na makusanyo," amesema Malima.
Hata hivyo, ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Butiama inalaumiwa kwa kuchelewa kumaliza ukaguzi wa viongozi wa Irasanilo waliotuhumiwa kwa ufujaji wa fedha za kikundi. Hadi sasa, ni miezi kumi, ofisi hiyo haijatoa ripoti ya uchunguzi wala kuwawajibisha waliobainika kuwa na makosa.
Kuchelewa kwa ripoti hiyo kumefanya viongozi wa muda kuendelea kushika nafasi hizo, jambo ambalo limekisorotesha kikundi, kwani viongozi wa mpito, akiwemo Mwenyekiti na Katibu, wamepewa mipaka ya majukumu, jambo ambalo linarudisha nyuma ufanisi wa kazi.


