Fahamu Taratibu za Kupata Mikopo wa Kununua Vifaa Vya Solar Kwa Ajili ya Miradi yako Toka NMB Bank Tawi la Musoma

GEORGE MARATO TV
0



Na Emmanuel Chibasa-Musoma

Changamoto ya ukosefu wa fedha kwa wakulima wadogo katika wilaya ya Musoma Mkoani Mara, inatajwa kuwa sababu kubwa inayoplelekea kushindwa kumudu gharama ya kununua vifaa vya nishati ya umeme jua, kwa ajili ya shughuli za kilimo cha umwagiliaji na kusababisha chakula kinachozalishwa  kupotea baada ya mavuno kutokana na uhaba wa uhifadhi baridi na miundombinu duni ya usafirishaji, pamoja na ongezeko la joto linalochochewa na mabadiliko ya hali ya hewa.

Pia kukosekana Miradi inayotekelezwa na Kampuni za nishati ya jua katika wilaya ya Musoma kunachangia wakulima wadogo kuendelea kupoteza mazao ya Kilimo na Uvuvi baada ya mavuno kutoka na kukosa miradi inayoweza kuwasaidia  teknolojia  na vyumba vya uhifadhi wa baridi vinavyoendeshwa kwa nishati ya jua bila kuhitaji kuunganishwa kwenye gridi ya taifa, ili kulinda chakula baada ya mavuno hali inayochangia kuathiri mapato ya wakulima pamoja na uhaba wa chakula.

Inaelezwa kuwa, endapo  pampu zinazotumia nishati ya umeme jua zingekua zinapatikana kwa gharama nafuu kwa wakulima wadogo katika bara la Africa,  basi wakulima milioni 7 wangeweza kuongeza wingi wa mavuno angalau  kwa 30% na kusaidia kupunguza matumizi  ya pampu za maji Zinazotumia mafuta ya dizeli na kuepuka tani milioni 197 za uzalishaji wa CO2, na hii ni sawa na kuondoa magari ya petroli zaidi ya milioni 46 barabarani kwa mwaka mmoja, ambapo pia wakulima wangeweza kuokoa Dola za Marekani bilioni 50 kwenye gharama za mafuta.

Taasisi za kifedha ikiwa ni pamoja na benki za ndani zinatajwa kusaidia kutatua changamoto hizo kwa wakulima wadogo kwa kutoa mikopo kwa watumiaji wa mwisho wa teknolojia za vifaa vya nishati ya umeme jua, Lakini upatikanaji wa fedha  kwa wakulima wadogo, bado ni changamoto licha ya uwepo wa uhitaji mkubwa toka kwa wakulima hao ili kuweza kulima kilimo cha tija.

WAKULIMA WANAVYOSEMA KUHUSU UPATIKANAJI WA MIKOPO

Deus Gondela mkulima mkazi wa Musoma Vijijini anasema kwa wakulima wadogo kupata fedha benki ni changamoto licha ya kuwa na dhamana ya mashamba wanayotumia kulima mazao ya chakula na biashara, lakini bado taasisi za benki haziwaamini huku taasisi nyingine za fedha wanapoweza kupata mikopo zikiwa na riba kubwa.

“ Sisi wakulima wadogo bado hawatuamini huko kwenye mabenki, niliwahi kwenda benki kuomba mkopo kwa ajili ya kulendeleza kilimo changu lakini alikuja mfanyakazi kutembelea eneo langu na kunihoji maswali na mwisho aliniambia ni vigumu kupata mkopo kwa sababu sikua na vielelezo vinavyoonesha mwenendo wa kilimo change katika kuingiza kipato” Amesema Deus

Joseph Okaka mkulima mkazi wa kijiji cha Bugwema Musoma Vijijini anasema licha ya serikali kuhamasisha wakulima wajiunge katika vikundi, ili waweze kupata mikopo katika taasisi za fedha kwa ajili ya kusaidia kuendesha shughuli zao za kilimo, lakini changamoto inayojitokeza ni baadhi ya wanakikundi kutokua waaminifu katika kurejesha fedha za mikopo hali inayopelekea benki kushindwa kuendelea kuwapa mikopo.


“Mimi binafsi naona kukosekana kwa uaminifu kati yetu ndio sababu tunakosa fursa za mikopo, mfano hapa kijijini sisi kama wakulima wa kilimo cha umwagiliaji hatuna kikundi na kila mtu analima kwa uwezo wake na anajua mwenyewe jinsi ya kujitafutia fedha kutokana na kukosekana kwa uaminifu kati yetu lakini pia hizo benki nazo haziji kututembelea ili ziweze kutusaidia hata kwa mkulima mmoja mmoja” Amesema Okaka.

Naye Loyce Joshua mkulima wa shamba la mboga mboga katika kijiji cha Bugwema anasema kutokana na kukosa mafaniko katika kilimo cha umwagiliaji kwa kutumia pampu za mafuta kunamfanya ashindwe kukopa fedha kwenye taasisi za fedha kutokana na kutojua namna nzuri ya kurejesha fedha hizo huku Penina Marcus akieleza uhitaji wa mafunzo ya maswala ya fedha na uwezeshwaji wa fedha zisizo na riba ili kwanza waweze kukua na kuimaisha uchumi katika shughuli zao za kilimo cha umwagiliaji.


UPATIKANAJI WA MIKOPO BENKI

Hali ya Upatikanaji wa mikopo Kwa wakulima wadogo  katika benki hapa nchini inaelezwa kuwa bado ni changamoto kutokana na masharti yanayowekwa na Benki.

Wakulima wadogo nao bado wanahitaji kubwa la fedha  kwa ajili Kusaidia kuendeleza shughuli zao za kilimo Ikiwa ni pamoja na kumudu gharama ya kununua vifaa vya nishati ya umeme jua lakini wanashindwa, hali inayopelekea wakulima wengi kushindwa kutumia teknolojia hiyo sababu  gharama nyingi ziko kwa watumiaji wa mwisho kama wauzaji wa vifaa na wakulima wadogo.

Sopeter Justin ni meneja wa NMB Bank tawi la Musoma, anasema katika benki hiyo wanatoa mikopo kwa wakulima na kuna mtaalam ambaye anahusika kushughulikia maswala ya wakulima.

Anasema changamoto kubwa kwa wakulima wadogo kushindwa kupata mikopo benki ni kutokana na wakulima wadogo kutokua na utaratibu wa kuweka kumbukumbu ya jinsi ya wanavyoendesha shughuli zao za kilimo pamoja na kutokua na utaratibu wa kutunza fedha zao benki pindi wanapovuna na kuuza mazao yao.

Ameongeza kuwa kutokana na wakulima kutokua na akaunti benki inawapa wakati mgumu kutambua kiasi cha Fedha anachopata Katika shughuli zake za kilimo  ili aweze kukadiriwa kiasi kinachaweza kukopeshwa na kumsaidia kuendesha shughuli zake lakini pia kurejesha fedha za mkopo bila Changamoto yeyote.

“ Sisi kama benki ya NMB tuko tayari kumkopesha mkulima au mtu yeyote anaehitaji kuwekeza kwenye nishati ya umeme jua katika miradi ya kilimo, uvuvi na hata uzalishaji mwingine lakini unakuta mkulima anakuja kufuata huduma ya mkopo anahitaji mfano kukopa milioni tano, unaenda kumtembelea kweli unakuta ana shamba lakini ukimuliza akuoneshe rekodi jinsi anavyouza mazao yake unakuta hana, ukimwambia tunahitaji tuone rekodi za fedha katika akaunti yako unakuta pia hana.

Mkulima huyu anakwambia we nipe tu mkopo ntaweza kurudisha fedha, Hii ndio changamoto kubwa kwa wakulima wadogo katika kupata mikopo benki." Amesema Sospeter

Nawaomba wakulima katika mkoa wa Mara wanaohitaji kuwekeza kwenye miradi ya nishati ya umeme jua waje tuwahudumie fedha zipo, Wakulima wadogo nawaomba waanze kujenga utaratibu wa kuweka rekodi ya shughuli zao za kilimo katika maandishi lakini pia wafungue akaunti  ambazo watakua wanatumia kuweka na  kutoa fedha pindi wanapouza mazao yao ili kutuweza kufahamu mzunguko wa fedha zake utakaotuwezesha kufahamu kiasi cha fedha anacho stahili kukopa” Amesema Sospeter


USHAURI WA WADAU KWA BENKI KUHUSU MIKOPO

Majura Maingu ni Meneja wa shirika la Victoria Fishing and Farming Organization(VIFAFIO) lenye makao yake makuu katika halimashauri ya manispaa ya Musoma, anasema benki nyingi hapa nchini zimekua zikiogopa kuwakopesha wakulima kutokana na kutokua na uhakakika wa kurejesha fedha zao, kutokana na changamoto mbalimbali zinazokuwa zinawakabili wakulima ikiwa ni pamoja na mabadiriko ya hali ya hewa inayopelekea mkulima kutokua na uhakika wa kupata mavuno.

Pia anasema wakulima wengi katika maeneo ya vijijini wanaendesha shughuli za kilimo katika mashamba ya familia na moja ya hitaji kuu la benki katika kupata mkopo ni lazima uwe na dhamana. Hali hii inapelekea kushindwa kutimiza masharti ya benki huku changamoto nyingine akisema ni taasisi za benki kutoruhusu pia mifugo kutumika kama dhamana.

“ Ushauri wangu kwa Benki mbali  na kuangalia dhamana ya eneo la mkulima wangeweka pia utaratibu wa wakulima wenye katika vikundi kuwadhini wenzao ili kusaidia kurahisisha upatikanaji wa mikopo kwa urahisi ili kurahisisha kuwafikia wakulima wengi zaidi na ambao pia wantumia mashamba ya familia na wanashindwa kuweka dhamana ya mashamba.” Amesema Majura

Ukuaji wa matumizi ya teknolojia ya nishati ya jua yataongezeka kwa kasi endapo wakulima na watumiaji wa nishati ya umeme jua watapata vifaa kwa ghrama nafuu hasa katika maeneo ya vijijini na ukuaji wake unategemea watumiaji wa mwisho kumudu teknolojia hii ambao wengi wao kwa sasa. Hawawezi hali inayopelekea asilimia 90% ya wakulima Kusini mwa Jangwa la Sahara ambao wangeweza kufaidika na pampu za maji  zinazotumia nishati ya za jua hawawezi kumudu kutokana na gharama za juu za awali au ukosefu wa mikopo.



Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
Post a Comment (0)

#buttons=(Accept !) #days=(20)

Our website uses cookies to enhance your experience. Learn More
Accept !
To Top