Balozi wa Tanzania nchini Comoro,Saidi Yakubu amekutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Umoja wa Visiwa vya Comoro,Mheshimiwa Azali Assoumani.
Mheshimiwa Rais Azali amemkabidhi Balozi Yakubu ujumbe maalum kwenda kwa Rais Samia Suluhu Hassan na akielezwa kuridhishwa kwake na ushirikiano wa sekta za biashara na kijamii ulioko baina ya nchi hizo mbili.
Rais Azali pia alimueleza Balozi Yakubu kuwa ameshakutana na Marais wa Tanzania Hayati Ali Hassan Mwinyi,Hayati Benjamin Mkapa,Jakaya Kikwete,John Magufuli na sasa Rais Samia Suluhu Hassan na wote wameonesha upendo mkubwa kwa Comoro na anafurahi sasa makampuni ya Tanzania yanakuja kuwekeza Comoro.
Kwa upande wake Balozi Yakubu alishukuru kwa ushirikiano anaoupata toka kwa mamlaka mbali mbali za Comoro na kumueleza namna uwekezaji na biashara baina ya Tanzania na Comoro inavyoimarika katika siku za hivi karibuni.





