Jopo la majaji watu likiongozwa na Jaji Eric Ogola pia linajumuisha majaji Anthony Mrima na Freda Mugambi lilichanguliwa na Naibu Jaji Mkuu Philomena Mwilu kusikiliza kesi zote zenye kuhusiana na kuondolewa madarakani kwa Rigathi Gachagua.
Kupitia Wakili Adrian Kamotho, Ruto anadai kuwa Mahakama ya Juu Zaidi pekee ndiyo yenye mamlaka ya kusikiliza kesi hizo.
Kulingana na Rais William Ruto, mahakama inafaa kutupilia mbali kesi hizo akidai kuwa zimewasilishwa kinyume cha sheria na ni utumiaji mbaya wa mchakato wa mahakama.
Rais Ruto ameongeza kuwa kesi dhidi ya Rais au mtu anayetekeleza majukumu ya afisi ya Rais katika kipindi cha uongozi wake kuhusiana na jambo lolote lililofanywa au kutofanywa chini ya sheria ya Katiba ya Kenya 2010 haziwezi kufunguliwa katika mahakama yoyote tu.
Kwa sasa mahakama imeahirisha kikao chake hadi mwendo wa saa nane mchana saa za Afrika Mashariki na kutoa uamuzi iwapo jopo hilo lina uwezo wa kusikiliza kesi hizo.
Naibu Rais aliyeondolewa madarakani Rigathi Gachagua alikuwepo mahakamani.
