Waziri Bashe na Mbunge Mpina Wakubaliana Kuweka Kando Tofauti zao

GEORGE MARATO TV
0


Serikali imeahidi kurejesha kitalu cha kuzalisha mbegu za pamba kwenye Jimbo la Kisesa Wilayani Meatu Mkoani Simiyu pamoja na kuwapatia wakulima wa Jimbo hilo Ruzuku ya pembejeo ikiwemo dawa ya viududu wanaoshambulia pamba pamoja na mbegu bora za pamba. 

Waziri wa Kilimo Hussein Bashe  amebainisha hayo wakati akihutubia mkutano wa hadhara katika kijiji cha mwandoya wilayani Meatu. 

Bashe pia amekabidhi Matrekta 40 kwenye Jimbo la Kisesa na kuwataka Maafisa Ugani kuacha Kukaa mijini na Badala yake waende vijijini kuwasaidia wakulima utaalam utakaowawezesha kufikia malengo ya serikali ya kuzalisha Mazao ya chakula na biashara kwa tija. 

Akiwa Jimboni Kisesa,Waziri Bashe amekutana na Mbunge wa Jimbo hilo Luhaga Mpina ambaye amesema yuko tayari kuweka kando tofauti zake na Bashe na kuungana naye katika masuala ya maendeleo pamoja na shughuli za serikali. 

Mpina ametumia fursa hiyo kueleza kuwa yeye na Bashe wanazo tofauti zao  iliyowafikisha hadi Mahakamani Lakini yuko tayari kushirikiana naye katika masuala ya utendaji wa serikali. 

Kwa upande wake,Waziri Bashe amemtaka mbunge huyo kuacha siasa katika zao la Pamba kwa maslahi ya wananchi.

“Rais Samia amefanya kazi kubwa katika kilimo,Mpina amesema hapa na mimi nataka nisisitize tuweke mambo mengine pembeni,aache siasa na sitaki siasa katika zao la Pamba, nafahamu zipo changamoto lakini tulipotoka sio tulipo sitakubali mtu arudishe nyuma jitihada hizi wanaoteseka ni wananchi,”alisema Bashe na kuongeza.

“Nami leo nimesimikwa kuwa mtemi wa Kisesa hivyo Mpina akinitambia pale bungeni kwa kuingia na fimbo ya uchifu nami nitaingia na yangu,”amesema.

Naye Mkuu wa mkoa Simiyu Kenan  Kihongosi amemuhakikishia Waziri Bashe kuwa yeye ndio mwenye dhamana na mkoa huo, hivyo hawezi vumilia watu wanaongiza siasa kwenye masuala ya maendeleo.

“Nimetumwa kazi na Rais Dk. Samia, Simiyu ni ya kwanza ama ya pili katika kuzalisha pamba hivyo kwa wananchi ni zao la kiuchumi,sitaki wanasiasa watumie zao hilo kutafuta umaarufu shida zinazosemwa katika zao hilo si za kweli wananchi wa Kisesa msikubali kutumika,”amesema Kihongosi. 






Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
Post a Comment (0)

#buttons=(Accept !) #days=(20)

Our website uses cookies to enhance your experience. Learn More
Accept !
To Top