Waziri wa Kilimo Hussein Bashe amewaasa wafugaji wa jamii ya Wasukuma wanaoishi katika kata ya Ndalila Wilayani Songea, kuhakikisha kuwa wanaishi kwa amani na wakulima wa jamii zingine wilayani humo.
Bashe amesema hayo akiwa katika kata ya Njalila Wilayani Songea wakati wa mwendelezo wa ziara yake kukagua miradi ya kilimo katika mikoa mbalimbali nchini ambapo amezungumza na wananchi kuhusu kero zao na mipango ya serikali katika kutatua kero hizo.
Ameelekeza viongozi wa taasisi za serikali kuchukua hatua na kufanya usanifu wa barabara na bwawa kwa ajili ya kumwagilia hekari 6000, pamoja na kujenga zahanati na kituo cha afya.
“Mkurugenzi wa Umwagiliaji na mhandisi wa Umwagiliaji mkoa pia yupo hapa, Kwa mwaka huu tutaanza na usanifu ambapo wataalamu watakuja kwa ajili ya kujua gharama, na masuala mengine muhimu kabla ya Kuanza utekelezaji”, alisema Bashe na kuongeza kuwa
”Serikali ifanye usanifu wa barabara kwa ushirikiano wa TARURA na Tume ya Taifa ya Umwagiliaji tutaanza usanifu kujua gharama za bwawa, barabara na ujenzi wa miundombinu ya shamba”
Aidha amebainisha mpango wa wizara kununua mazao kutoka kwa wakulima, kwa lengo la kuwaepusha wakulima na hasara za kuuza mazao yao kwa bei ya chini.
"Mwenyekiti wa Skimu kasema mnauza mpunga kwa elfu sitini kwa gunia, serikali itanunua gunia moja la kg 90 kwa shilingi 81,000 na serikali itaununua wote Mpunga” alisema Bashe.
Pia, alitembelea shamba la uzalishaji wa kahawa Avivi katika Kata ya Kilagano, wilaya ya Songea, na kuwasihi wawekezaji kuchangia maendeleo ya jamii kwa kuwachimbia visima vya umwagiliaji.
Bonde la mto Njalila lipo wilaya ya Songea, kata ya Kilagano, kijiji cha Kilagano na limepakana na wilaya ya Mbinga upande wa mashariki mwa bonde, linapatikana umbali wa kilometa 93 kutoka manispaa ya Songea, ambalo linatumika kwa shughuli za kijamii na kiuchumi kama kilimo cha mazao mchanganyiko ikiwemo mpunga, mahindi, ndizi, miwa, mbogamboga na ufugaji.