Waziri wa Kilimo Hussein Bashe (mb) amepiga marufuku wafanyabiashara wanaonunua kahawa kwa njia ya Kangomba na kuagiza wakamatwe huku akisisitiza kuwa uwekezaji mkubwa unaofanywa katika zao hilo umelenga kuteka soko la kahawa ya Tanzania kimataifa.
Amesisitiza kuwa serikali kwa sasa inawekeza katika kahawa kwa kugawa miche na mbolea ya ruzuku hivyo, anatarajia kupigwa vita na wafanyabiashara kutokana na kukemea kangomba lakini hatarudi nyuma kwa maslahi ya zao hilo.
Waziri Bashe amesema hayo wakati wa kutembelea mashamba, viwanda vya kuchakata kahawa na skimu za umwagiliaji kwenye wilaya za Mbinga na Nyasa.
“Najua haya maamuzi yatakuwa na maumivu na yatakuwa na kelele, mimi kelele nimezoea, kamateni wanaonunu kahawa kwa kangomba"alisema Bashe na kuongeza kuwa
“Tutegemee kelele nyingi kutoka kwa wafanyabiashara lakini sipo tayari kuona kangomba katika kahawa.Kelele zitakuwa nyingi watapitishia kwa wakulima tujiandae lakini nasema ili kufikia soko la kimataifa hatuwezi kuvumilia ununuzi usiofaa,”
Waziri Bashe amesisitiza kuwa hatua ya serikali kuwekeza katika zao la kahawa imelenga kuijengea ubora kahawa ya Tanzania kimataifa na kunufaisha wakulima.
“Tunatoa mbolea na miche kwa ruzuku na kuwezesha kilimo hiki kuhimili ushindani dhidi ya kahawa za nchi nyingine,”amesema.
Akiwa katika miradi ya umwagiliaji inayotekelezwa na Tume ya Taifa ya Umwagiliaji Waziri Bashe amesema serikali imeshampata mkandarasi kwa skimu zenye hekta 8395 ambapo miundombinu mbalimbali itajengwa barabara za ndani ya shamba, madaraja na vigawa maji ndani ya shamba na tayari usanifu umeshakamilika.
Pia Waziri Bashe ameitaka Tume hiyo kufanya usanifu na kuziingiza barabara za Lipingo katika mpango wa utekelezaji wa mradi huo wa Umwagiliaji
Aidha ameitaka Tume ya Taifa ya Umwagiliaji kujenga ghala katika eneo la mradi na mashine ya kukoboa mpunga ili wananchi waweze kuuza mchele badala ya Mpunga.
Ameongeza kuwa Wizara ina mpango wa kuanza uzalishaji wa mbegu karibu na eneo la mradi wa Lundo,kuanzisha vituo vya zana za kilimo pamoja na kujenga kituo cha mbolea kwenye eneo hilo.
Naye, Mbunge wa Jimbo la Nyasa Mhandisi Stella Manyanya, amesema Wilaya hiyo inahitaji kukua kiuchumi na tegemeo kubwa ni kilimo cha mpunga hivyo wanatarajia miradi ya umwagiliaji iwe chachu ya uzalishaji.