Mamia ya wajasiriamali wanawake na vijana kutoka kata ya Mabuki wilayani Misungwi Mkoani Mwanza wamenufaika na Mafunzo yanayolenga kuwajengea uwezo wa namna ya kujikwamua kiuchumi.
Mafunzo hayo yametolewa na Benki ya CRDB kupitia Progam ya Imbeju inayolenga kuwawezesha akinamama na vijana kuweza kupata mitaji wezeshi.
Akizungumza katika mafunzo hayo,Msimamizi wa biashara wa Benki ya Crdb kanda ya ziwa May Mosi Ndunguru amesema kuwa program hiyo imebuniwa na benki hiyo kwa ajili ya kuwezesha wajasiriamali vijana na wanawake kuweza kupata mitaji wenzeshi ili kukuza biashara zao.
Naye mhamasishaji na mwezeshaji wa Benki ya Crdb Misungwi Angela Palangyo amesema kuwa Program Imbeju inatoa uwezeshaji wa kati ya shilingi millioni moja na millioni 30.
Palangyo amesema kuwa vigezo vya kupata uwezeshaji huo ni pamoja na kuwa mtanzania mjasiriamali ambaye amefanyia kazi wazo lake ambapo Benki hiyo baada ya kuona uthubutu,mhusika hupatiwa uwezeshaji ili aweze kukuza na kuendeleza ubunifu wake
Kwa upande wao,Wajasiriamali walionufaika na mafunzo hayo wamesema kuwa yamewapa mwanga mpya wa namna ya kupata mitaji ya kukuza biashara zao.
Mmoja wa wajasiriamali hao Asha Shigi na Simon Mashimba wamesema kuwa wanategemea kupata mitaji kutoka kwenye Taasisi zinazotoa mikopo umiza na hivyo kuchangia biashara zao kutokuwa na tija
Meneja wa benki ya Crdb Misungwi Deogratius Kessy ameviasa vikundi vya vijana na Wanawake wajasiriamali kuweka akiba zao benki ili kuimarisha usalama wa fedha badala ya kuhifadhi majumbani.
Wajasirimali hao wamesema kuwa ujio wa program ya Imbeju ni mkombozi kwao kutokana na mikopo inayotolewa na Halmashauri kutowafikia wahitaji wote.
Mgeni rasmi katika mafunzo hayo ni Afisa Tarafa ya Misungwi Peter Michael ambaye amewaasa watanzania kujenga mazoea ya kuweka akiba benki na kutumia benki kwa shughuli halali za kifedha.
Michael amewahimiza wajasirimali kutoogopa kukopa fedha benki ili kukuza mitaji yao sanjari na kuhakikisha kuwa wanarejesha mikopo hiyo kwa wakati ili kuwezesha watu wengi zaidi kunufaika na fursa zinazotolewa na Mabenki
“Uwepo wa Benki ya Crdb hapa Misungwi umeongeza urahisi wa upatikanaji wa mikopo kwa wananchi ikiwemo mikopo ya biashara na kilimo,hivyo basi ni muhimu kwa wafanyabiashara,wajasiriamali na wateja wa kada nyingine kuchangamkia fursa hii,nitoe rai kwenu benki ya Crdb kuweka masharti na vigezo nafuu ikiwemo kutoza riba ndogo ili watu wengi zaidi waweze kujitokeza na kunufaika na mikopo hii na kuachana na mikopo umiza”alisema Michael
Pia amewahimiza maafisa maendeleo ya Jamii kutembelea wananchi waishio vijiji ili kuwahamasisha na kuwapa elimu na kuwasaidia namna ya kuunda na kusajili vikundi vitakavyowasaidia kupata mikopo.
Zaidi ya vikundi 19 vya akinamama na vijana kutoka wilaya ya Misungwi vimepatiwa elimu ya uwezeshaji wa kifedha inayolenga kuwajenga kujikwamua kiuchumi katika kujiongezea kipato.