Na Dawati la Habari NIRC Ruvuma
Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan amesema mafanikio yaliyopo sekta ya kilimo hayatokei kwa bahati mbaya bali ni kutokana na uwekezaji mkubwa unaofaywa na serikali kwenye sekta hiyo
Samia amesema kuwa Uwekezaji huo umewezesha kuongezeka kwa uzalishaji wa zao la kahawa kwenye shamba la AVIV kutoka tani 65 hadi kufikia tani 85 katika kipindi cha mitatu iliyopita,ongezeko hilo limeliingizia Taifa dola za kimarekani milioni 250.
Ameitaka Wizara ya Kilimo kuhakikisha wawekezaji waliopo mbali wanayoyafanya katika kurudisha kwa jamii pia wahusike katika kurithisha ujuzi na teknolojia hususani za Umwagiliaji zinazotumika katika sekta hiyo ili kuwezesha wananchi kuwa na kilimo chenye tija kwa maslahi ya kizazi cha sasa na vijavyo.
Rais Samia amesema hayo alipotembelea shamba la uzalishaji wa Kahawa la AVIV mara baada ya uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi wa maghala 28 ya kuhifadhi mazao ya nafaka yaliyo chini ya Wakala wa hifadhi ya Chakula (NFRA) Wilayani Songea Mkoani Ruvuma katika muendelezo wa ziara yake ya siku sita mkoani humo.
Rais Samia ametaka wakulima wa kahawa nchini watumie fursa ya kupanda kwa bei ya kahawa kuhifadhi fedha ili wasitaabike kipindi bei itakaposhuka
“Misimu ikiwa mizuri na bei ikiwa nzuri tuwe na mifumo ya kujiwekea akiba ili mabadiliko ya tabia nchi yanapotokea tuwe na Akiba,” amesema.
Aidha ameielekeza Wizara ya Kilimo kujipanga vyema na masharti yanayotolewa na masoko ya kimataifa ya kahawa hasa lile la uzalishaji bila kukata misitu,kukagua, kuyasajili na kupeleka taarifa za mashamba kwenye masoko hayo ili ijulikane linakotoka zao husika.
“Wanatambua tusikate misitu,kule kwao wameshakata lakini sisi tunataka soko, tunapaswa kuhakikisha tunayatimiza masharti ili kupata soko,” amesema Rais Samia
Pia ameagiza wizara kufanya uchunguzi wa madai ya wakulima wa kahawa kukatwa fedha kinyemela na vyama vikuu vya ushirika.
“Ninatambua uwepo wa malalamiko ya wananchi kwamba kwa sababu kahawa imepanda bei baadhi ya vyama vikuu vya ushirika (hakuvitaja) vinawakata wakulima kinyemela,” amesema.
Rais Samia amemtaka Waziri Bashe kuhakikisha mfumo uliopo unakuwa wa wazi ili kuwezesha wakulima kuona wanachouza na uhalisia wa makato yao.
“Huu ujanja ujanja unaoendelea unapaswa kukomeshwa,” amesema Mkuu huyo wa nchi alipotembelea shamba hilo lenye ukubwa wa hekta 200"
Katika hatua nyingine, Rais Samia ameutaka uongozi wa shamba hilo,kufanya shughuli za kijamii ikiwemo kujikita katika uchimbaji wa visima vya umwagiliaji kwenye mashamba ya wakulima ili wakulima waweze kuzalisha kahawa kwa tija na kuuza kwa Aviv.
Awali, akizungumza katika ziara hiyo, Waziri wa Kilimo Hussein Bashe amesema shamba hilo ni moja kati ya 50 yanayozalisha kahawa na kwamba hilo ni kubwa zaidi ya mengine yote.
Bashe, amesema asilimia 60 ya kahawa inayozalishwa na shamba hilo inauzwa nje ya nchi kwa Kampuni ya Strabag.
Hata hivyo, amesema wastani wa bei ya kahawa mwaka huu ni Dola 4.3 za Marekani, kiwango ambacho ni tofauti na nyakati zilizopita.
"Mafanikio yaliyopo kwenye sekta ya kilimo yametokana na maamuzi ya kisera na sheria ya Rais Dkt. Samia hususani katika kuboresha sekta ya uwekezaji na kurudisha masoko"alisema waziri Bashe na kuongeza kuwa
“Hali hii imerudisha uhai wa uzalishaji kwa wawekezaji na wakulima wa ndani,shamba hili linategemea zaidi shughuli za umwagiliaji hivyo Wizara tumemuagiza muwekezaji uchimbaji wa visima na mabwawa unufaishe jamii katika mashamba ya wananchi,”
Shamba la AVIV Tanzania Ltd ni moja kati ya mashamba 50 makubwa yanayozalisha kahawa nchini, likiwa na zaidi ya hekta 2,000, ambapo zaidi ya hekta 1,000 zimeshapandwa kahawa.
Kwa Mujibu wa Bashe, Maghala 28 ya kuhifadhia mazao ya nafaka yenye thamani ya shilingi bilioni 527 yanajengwa mkoani Ruvuma na yatakuwa na uwezo wa kuhifadhi tanı 1,000 kila moja.

Naye Mbunge wa Jimbo la Peramiho, Jenista Mhagama, ameishukuru serikali kwa maamuzi ya kisera yanayovutia uwekezaji na kuongeza uzalishaji wa mazao mbalimbali.
Ameeleza kuwa mradi wa AVIV umekuwa na faida nyingi kwa jamii, na mwekezaji ameshirikiana na uongozi wa serikali kuandaa mpango wa urithishaji wa mchakato wa kilimo cha kahawa huku Mwekezaji huyo akichangia hadi bilioni moja kwa halmashauri ya Peramiho










Comments
Post a Comment